HIVI karibuni, ulimwengu wa soka duniani kote ulipata mshangao baada ya nyota wa zamani wa Barcelona na Timu ya Taifa ya Brazil, Ronaldinho De Assis Moreira maarufu kama Ronaldinho Gaucho kukutwa na hatia ya kutumia hati feki ya kusafiria kuingia nchini Paraguay.

Ronaldinho na kaka yake aitwaye Roberto ambaye pia ni meneja wake katika masuala ya biashara, walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi kabla ya kufikishwa mahakamani ili kusikiliza mashitaka hayo.

Juhudi mbalimbali zinafanyika ili kuhakikisha Ronaldinho aliyekiri kosa anamalizana na soo hilo, lakini bado staa huyo yuko kwenye hatari ya kukumbana na kifungo iwapo mahakama itajiridhisha kuhusu shauri hilo.

Licha ya kwamba kwa sasa yupo nje baada ya kupata dhamana bado kuna jambo la kujifunza katika hili kwa wachezaji wetu.

Kwa upande wangu nadhani kisa hiki cha mkongwe huyu wa soka kina mengi ya kuwafundisha nyota wetu hapa nchini kwani wachezaji wengi ambao wanapata bahati ya kufanya vizuri na kuwa katika viwango vya juu hupata upofu wa ustaa na kusahau kuwa kuna maisha baada ya majina makubwa na ustaa walionao.

Sekeseke hili la Ronaldinho liwakumbushe wachezaji wetu kuwa licha ya ustaa walionao uwanjani, mitandaoni na kwenye media bado wanabaki kuwa binadamu kama wengine na lolote linaweza kuwakuta.

Ni nani alidhani kuwa mshindi huyo wa Ballon d’Or mbili na umaarufu, heshima yake angeweza kuwa mahabusu kwa muda kwa ishu ya paspoti?

Unakuta huku kwetu mchezaji eti kwa kuwa tu anacheza Ligi Kuu, anajulikana kwenye viwanja vya bata na kupata ‘dm’ za kutosha za wadada wa mjini mitandaoni basi anasahau kabisa hata kujiwekeza kwa maisha ya baadaye, mwishowe anapokuja kuachana na soka anajikuta kabaki mwenyewe huku wale wote waliokuwa wakitumbua pamoja wamepotea.

Ni muhimu wachezaji wetu wakakumbuka msemo usemao “fainali uzeeni” hivyo wanapaswa kuchagua washauri na wasimamizi sahihi katika mambo yao binafsi kipindi hiki wakiwa wanatengeneza pesa ya kutosha.

Mchezaji unaposema ‘role model’ wako ni Cristiano Ronaldo au David Beckham usiige tu mikimbio yao uwanjani, unadhifu wao, au jinsi wanavyotanua na vimwana huko Dubai na fukwe za Ibiza, bali hakikisha unaiga na akili ya uwekezaji ambayo tunaiona kwa nyota hao ambao ni dhahiri kwa uwekezaji wanaoufanya sasa shida za uzeeni watabaki kuzisikia kwa wengine tu.

Mara kadhaa tumeshuhudia wachezaji ambao walitamba enzi hizo katika soka hapa nchini wakiadhirika na kuwa ombaomba katika uzee wao huku wengi wao wakitoa sababu ya malipo madogo waliyokuwa wakipata.

Lakini bado hatuwezi kuficha ukweli pia kuwa kuna baadhi yao ambao macho yao yalifumbwa na ustaa wakajua kuwa watazeeka nao kumbe ustaa ni jambo la kupita tu.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.