TUPO nyakati ngumu kwa sasa hilo lipo wazi kutokana na ganzi ambayo imetanda kwenye mioyo ya watu wote.
Tunaona na kuskia taarifa kila siku kuhusu ndugu zetu, rafiki zetu na jamaa pia wakiumia kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Ni kweli inaumiza na inahuzunisha pia lakini hakuna namna ya kufanya kwa sasa zaidi ya kuchukua tahadhari kwani Virusi vipo mtaani.
Tanzania yetu na dunia nzima kiujumla inapambana kutafuta suluhisho la Virusi vya Corona kwani hakuna Serikali inayopenda kuona watu wake wakiangamia.
Kwenye familia ya michezo pia mambo bado hayajakaa sawa kwani kila iitwapo leo watu wanakumbuka burudani ndani ya uwanja.
Ni ngumu kuamini kwamba mambo yamebadilika ila kweli habari ndio hiyo na ni lazima tuipokee ili tuitendee kazi kwa ukamilifu.
Bado rai yangu ipo kwa Tanzania kuwaomba wazidi kuchukua tahadhari na kuongeza umakini katika kupambana na Virusi vya Corona.
Ukubwa wa tatizo lililo mbele yetu sio wa kutisha ila ni lazima tujitoe kupambana kupata njia ya kutoka ili maisha yaendelee.
Wapo ambao wanapenda kusambaza taarifa kuhusu Virusi vya Corona ilhali hawana mamlamka na wakati mwingine wanapotosha habari zao.
Kwa hawa wenye tabia hii ikiwa wapo kwenye familia ya michezo wanapaswa waache mara moja kwani hili janga halihitaji utani hata kidogo.
Ni janga ambalo linahitaji umakini mkubwa katika kupambana nalo na kutafuta majibu ya tatizo ambalo lipo kwa sasa.
Wote tunapaswa tuungane wote kupambana na Virusi vya Corona imani yetu ni kwamba hali itarejea kuwa shwari iwapo tutaunganisha nguvu zetu.
Wahenga walisema kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu hivyo tuwe na umoja katika hili.
Kwenye ulimwengu wa michezo ligi nyingi zimesimama na kwa sasa hakuna kinachoendelea ni kama vile kwa sasa tupo likizo.
Ila kwa wakati huu bado ninaendelea kusisitiza na kuwakumbusha wachezaji kwamba ni muhimu kulinda vipaji vyao kwa kuwa wanategemewa kuokoa jahazi kwenye timu zao.
Pia wapo wale ambao wamepewa katazo la kupunguza aina ya vyakula ambavyo kitaalamu vinaongeza uzito hilo nalo ni muhimu pia.
Yote kwa yote ni muhimu kuona kwamba kila mmoja anachukua tahadhari hata akiwa yupo kwenye mazoezi itasaidia kumlinda yeye na familia yake pia.
Kila mchezaji ana nafasi ya kuwa balozi mzuri kwa kufanya yale ambayo yanaelekezwa na Serikali pamoja na wizara ya afya.
Ukiachana na masuala ya kulinda vipaji pia kwa sasa kumekuwa masuala ya timu kufanya tathimini ya pale ambapo zilikwama kabla ya ligi kusimama.
Hili pia lisipuuzwe lifanywe kwa umakini lakini tahadhari pia ichukuliwe katika kujilinda wakati wa viko hivyo.
Tusifikiri kwamba tupo salama kiasi kikubwa hapana ni Mungu tu anatufanyia amani hivyo nasi tuendekee kuomba dua ili tubaki salama na maisha yaendelee bila maumivu makubwa.
Muda wa kutengeneza ripoti maalumu ambazo zitakuwa mwongozo kwa ajili ya wakati ujao ni muhimu kufanywa taratibu na kwa umakini mkubwa hii itasaidia benchi la ufundi kujua malengo yao ya baadaye.
Itapendeza kuona kwamba kila mwanafamilia ya michezo kwenye timu akitoa mchango wake na kusikilizwa kwa umakini ili kujenga umoja ndani ya klabu.
Haitapendeza kwa wakati huu iwapo kuna mmoja atakuwa na sauti yenye mamlaka huku wengine wakiwa hawapewi nafasi ya kusikilizwa hiyo sio sawa.
Kile ambacho kinafikiriwa kwa sasa ni namna gani ligi itarejea na hatma yake itakuaje lakini katika hili tusiumize sana kichwa tunachotakiwa kuumiza kichwa chetu ni kwenye dua hali iwe salama.
Imani yangu ni kwamba iwapo hali itakuwa salama hata leo basi Serikali ambayo ndio ilitoa tamko basi itatoa ruhusa ya kuendelea na maisha yake ambayo tulikuwa tunayaishi wakati ule kabla ya Virusi vya Corona.
Hakuna ambaye hajakumbuka maisha ya ushindani kwenye Ligi Kuu Bara, Ligi ya Wanawake Ligi Daraja la Kwanza ilikuwa ni moto ambao unaendelea ila hakuna namna ya kufanya kwa sasa.
Wale ambao bado wanapuuzia kanuni za afya ninapenda kuwaomba wasifaye hivyo wafuate kanuni za afya ili maisha yaendelee na kazi kubwa kwao iwe kuchukua tahadhari.
Iwapo wao watachukua tahadhari watawaokoa wale ambao hawakuwa na hatia ya kupata Virusi hivyo ikiwa ni pamoja na watoto na akina mama wanaoshinda nyumbani na familia zao kiujumla.
Post a Comment