KIUNGO wa Simba, Gerson Fraga, amethibitisha kuwa yeye ni Mbrazil halisi, baada ya jana kuweka nyavuni mabao yote mawili katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi Coastal Union uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa ushindi wa bao 2-0.
Katika mchezo huo uliochezwa muda mchache baada ya mvua kunyesha Fraga alifunga bao la kwanza dakika ya saba, kwa mpira wa kichwa akiwa ndani ya eneo la goli akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo, Clatous Chama ambaye jana alikuwa mwiba kwa wapinzani wao.
Fraga tena aliwainua mashabiki wa Simba dakika ya 78, baada ya kufunga bao la pili kwa mpira uliotemwa na kipa wa Coastal Union, Soud Dondola, shuti lililopigwa na kiungo Hassan Dilunga aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajib.
Ufundi na utulivu kwa wachezaji ulikosekana katika mchezo huo, baada ya uwanja kuwa na maji maji, na kufanya timu zote mbili kucheza mipira ya juu hasa katika kipindi cha kwanza.
Kwa matokeo hayo Simba inaendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 47, katika michezo 18 kwa pointi 11 zaidi ya Azam FC wanaofuatia katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 36 katika mechi 17 na Coastal Union inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 30, baada ya kucheza michezo 18.
Mechi nyingine za ligi kuu leo, JKT Tanzania na Polisi Tanzania ilisitishwa dakika ya 53 kufuatia Uwanja wa Uhuru kujaa maji na mpaka mchezo unaahirishwa walikuwa hawajafungana na mchezo kati ya Tanzania Prisons na KMC haukufanyika kabisa sababu ya mvua kubwa.
Kagera Sugar iliifunga Singida United kwa 3-0 katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mabao yoye yakifungwa na Kelvin Sabato na katika Uwanja wa Majaliwa Namungo FC iliibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Mbao FC, mabao mawili yakifungwa na Reliants Lusajo na Hashim Manyanya na Ndanda ikicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona iliifunga Alliance FC kwa bao 1-0 lililofungwa na Vitalis Mayanga, Biashara United iliifunga Mwadui FC kwa mabao 2-1 yakifungwa na Mpapi Nasibu na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ lile la Mbao lilifungwa na Mussa Chamgenga na Ruvu Shooting ikaichapa Lipuli FC 3-1 na mabao yake yakifungwa na Graham Naftari, Rajab Zahir na Sadat Mohamed huku bao la Lipuli likifungwa na Daruweshi Saliboko
Post a Comment