KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vanderboeck raia wa Ubelgiji amekasirishwa na kitendo cha wachezaji wake kuwaruhusu wapinzani kuingia na mpira ndani ya 16, hivyo amepanga kuja na mbinu ya kuizuia.
Kocha huyo ameweka bayana hilo baada ya kikosi chake hicho kuruhusu mabao mawili wakati walipocheza na Namungo FC, juzi Jumatano na kufanya kikosi hicho kuruhusu mabao manne kwenye mechi zao tatu za mwisho walizocheza katika Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo ameliambia Championi Jumamosi, kuwa kwa sasa anaogopa sana mipira hiyo kwa sababu inazalisha mabao kwa upande wao lakini yuko kwenye mpango mkubwa wa kulitafutia dawa tatizo hilo kwenye mechi zao zijazo.
“Hatuwezi kuficha hilo kwamba tunafungwa mabao na tunaruhusu kwenye kila mechi zetu ambazo tumecheza hivi karibuni. Kila mpira unaoingia kwenye 16 yetu ni hatari kwetu, kwa sababu lazima turuhusu bao kama ilivyo kwenye mechi zilizopita na hii ya leo (juzi) Jumatano.
“Ila hilo tunalifanyia kazi na huko mbele nafikiri linaweza kumalizika, kitu kikubwa ambacho ninakifurahia ni kuona timu inakuwa na uwezo wa kupambana hadi dakika za mwisho kwa ajili ya kusaka bao.
“Hiyo imetokea kwenye mechi hii lakini hata mechi zetu za nyuma tulikuwa na ari kama hii ya kupambana hadi mwisho na ndiyo tukapata kujihakikishia pointi tatu,” alimaliza Sven
Post a Comment