WABUNGE wameitaka serikali kuwekeza katika michezo ili kuwapata wachezaji wengine wazuri kama nahodha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta ambaye hivi karibuni alisajiliwa na Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu England.
Samatta tayari ameanza kuitumikia timu yake hiyo mpya na Jumanne iliyopita alicheza mechi ya kwanza dhidi ya Leicester City na kupata ushindi wa mabao 2-1.
Wakiuliza maswali ya nyongeza bungeni jana, wabunge waliitaka serikali kuwekeza katika vifaa vya michezo na kuanzisha viwanja vya taaluma vya michezo.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia, alisema hivi sasa kuna mwamko mkubwa wa wazazi kutaka kushiriki katika michezo kutokana na kuchagizwa na mafanikio aliyoyapata Samatta.
“Lakini kuna tatizo kubwa la vifaa vya michezo, serikali ina mkakati gani kuhakikisha vifaa vinapatikana kwa urahisi,” alihoji Mtulia.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Cecil Paresso, alisema Watanzania wengi kwa sasa wanamshangilia Samatta kwa kusajiliwa na timu hiyo ya England, lakini ni wazi amesajiliwa kutokana na jitihada zake binafsi.
“Hii inatuambia tunaweza kuwa na kina Samatta wengi kama serikali ikiwezeka vya kutosha katika michezo, kwa nini serikali isianzishe kwenye majiji makubwa 'sports arena’,” alihoji.
Awali akijibu swali la Mbunge Mtulia, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, alikiri kuwapo na tatizo la vifaa vya michezo lakini wafanyabiashara wamekuwa wakihamasishwa kuagiza vifaa vya michezo kutoka nje ya nchi.
“Pia kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika viwanda vya kuchakata vifaa vya michezo,” alisema Shonza.
Akijibu swali la Mbunge Paresso, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema kutokana na juhudi za serikali na wananchi wenyewe, sasa hivi Tanzania ina wachezaji 22 wanacheza soka la kulipwa na si Samatta peke yake.
“Tumeona vipaji havipatikani ukubwani, vinapatikana kwa kuanzia utotoni na ndio maana kuna michezo ya Umishumita kwenye shule ili kukuza vipaji,” alisema Mwakyembe
Post a Comment