MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga, Mrundi Amissi Tambwe, leo au kesho anatarajiwa kutua nchini kwa ajili ya kwenda kumuona straika mpya wa timu hiyo, Bernard Morrison akiupanda mpira tena wakati timu hiyo ikivaana na Mtibwa Sugar.
Tambwe aliyejiunga na Yanga msimu wa 2014/15 akitokea Simba, aliondoka katika timu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2018/19, na akiwa Yanga alifanikiwa kuifungia mabao 52 kwenye ligi kuu.
Morrison ni mchezaji mpya ndani ya Yanga na mpaka sasa ameshacheza mechi mbili, amefunga bao moja na kutoa asisti mbili. Anasifika kwa mbwembwe nyingi uwanjani kama kupanda mpira na kupiga pasi bila kuangalia mpira unapoelekea, sasa hii ndiyo imemfanya Tambwe afunge safari kutoka Burundi mpaka Bongo.
Tambwe alisema kuwa, anatamani kumwona mchezaji huyo akiwa uwanjani baada ya kusikia sifa zake ndiyo maana ameamua kuja nchini kumwona atakapokuwa akipambana na Mtibwa Sugar kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
“Mbali na kuja kumuona mchezaji huyo pia nakuja kufuatilia mambo yangu klabuni hapo kwa sababu wakati naondoka ishu zangu nyingi zilikuwa hazijakaa sawa.
“Morrison nasikia ni mchezaji mzuri, sijawahi kumwona uwanjani kwa hiyo nataka nimwone ili niweze kukubaliana na maoni hayo ambayo nimekuwa nikipewa na baadhi ya watu kuwa jamaa ni mkali na kudai kama angekuja wakati mimi nipo basi ningefunga sana,” alisema Tambwe.
Post a Comment