Unaambiwa uongozi wa Klabu ya Yanga umefikia katika sehemu nzuri kuelekea kwenye mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji chini ya nguli wa mifumo ya soka la kisasa kutoka nchini Ureno, Antonio Domingos Pinto.
Klabu hiyo, wiki iliyopita ilimpokea Mreno huyo aliyekuja kwa ajili ya kufanya mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo na kikubwa ni kuanza mipango ya mabadiliko ya mfumo mpya wa klabu hiyo.
Yanga imepanga kupiga hatua katika klabu hiyo kwa kuhakikisha wanakwenda kwenye mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kama ilivyokuwa kwa Simba iliyo chini ya Mohammed Dewji ‘Mo’ ambayo hadi hivi sasa imejenga viwanja viwili vya kucheza soka, cha nyasi bandia na halisi huko Bunju jijini Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alisema kila kitu kilikwenda vizuri kati ya Mreno huyo na uongozi katika mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni kabla ya Mzungu huyo kurudi kwao kufuata baadhi ya vitu vyake.
Mwakalebela alisema kuwa wameshafikia muafaka juu ya suala hilo katika kuelekea mfumo wa mabadiliko yenye tija katika klabu hiyo iliyopanga kujenga viwanja vikubwa viwili vya mazoezi huko Kigamboni, Dar.
“Pinto alikuja kwa ajili ya mazungumzo ya awali ikiwemo kuiona Yanga ambayo inahitaji kufanya naye kazi na sisi kumfahamu na uzuri kila kitu kilikwenda vizuri.
“Mreno huyo tayari yupo kwao alipokwenda kwa ajili ya kuchukua mabegi yake na anatarajia kurejea hivi karibuni kuanza kazi hiyo ya kuelekea mfumo wa mabadiliko.
“Na mara ataporejea ataanza kazi haraka na kikubwa ni kuona klabu yetu inapata mafanikio kwa kupitia Mreno huyo ambaye tumeridhishwa na CV yake na tunataka aendeleze pale tulipoishia sisi viongozi,” alisema Mwakalebela.
Mwakalebela alisema kuwa Mreno huyo cheo chake kitakuwa ni Meneja Miradi ‘Project Manager’ ambaye yeye mara ataporejea nchini siku yoyote ndani ya wiki hii, atakuwa na timu yake ya watu kadhaa wenye weledi wa kufanya naye kazi.
“Sisi tumejaribu kuwa ‘kiprofesheno’ zaidi ya wenzetu waliotangulia katika mfumo wa mabadiliko kwa kumleta Mzungu atakayekuwa na timu yake itakayoitoa klabu yetu hapa tulipo na kwenda mbele zaidi.
“Timu hiyo ya Meneja Miradi itakuwa ikitupa sisi taarifa za wapi walipofikia katika kuelekea mfumo wa mabadiliko wa klabu yetu ya Yanga, tukiamini kwa kupitia yeye tutafanikiwa.
“Hivyo, Wanayanga wanachotakiwa hivi sasa ni kuwa watulivu viongozi wakimalizia hatua za mwisho za kubadili mfumo wa mabadiliko ya klabu yetu, lengo ni kuona tunapiga hatua zaidi ya hapa tulipofikia,” alisema Mwakalebela.
Aidha, jopo la mainjinia jana usiku lilitarajiwa kukutana kwa ajili ya kupitia kwa mara ya mwisho ramani ya viwanja vyao viwili watakavyovijenga huko Kigamboni, vitakavyokuwa vya nyasi bandia na halisi.
“Uwanja uliopangwa kujengwa Kigamboni ni wa nyasi halisi na bandia, hivyo wajumbe wa kamati ya utendaji watakutana na mainjinia leo Jumapili (juzi), badala ya Jumamosi (juzi) kwa ajili ya kuipitia ramani hiyo ya uwanja kwa mara ya mwisho.
“Katika kikao cha awali kilichofanyika wiki iliyopita, kilishauri kuongeza baadhi ya michoro inayotakiwa kuwepo kwenye ramani ya viwanja hivyo tulivyopanga kuvijenga.
“Katika kikao hicho wajumbe walishauri kuongeza idadi ya vyoo, mabafu na idadi ya hosteli ambayo tayari imekamilika hivyo wajumbe watakutana na mainjinia kwa ajili ya kuikagua katika hatua ya mwisho,” alisema Mwakalebela
Post a Comment