NA SALEH ALLY
NATAKA
niende moja kwa moja kuwa nimekuwa nikikerwa na propaganda zinazoenezwa
na baadhi ya watu ambao ninaamini wameshindwa mambo.
Mjadala
huu unachombezwa na baadhi ya mashabiki ambao wanaonekana wameshindwa
kujitambua, wameshindwa kuelewa kuwa wanatumika vibaya na baadhi ya
viongozi ambao wameshindwa majukumu yao.
Kuna
propaganda ambayo haina faida na afya ya mchezo wa soka nchini
kuendelea kulazimisha ionekane waamuzi wanaipendelea sana Simba.
Katika hali ya kawaida, mimi kama mdau wa mpira siwezi kuungana mkono hata kidogo na waamuzi ambao ningeona wana nia hiyo.
Kama
wangekuwa kweli wanaipendelea Simba, bila shaka tungepiga kelele na
kukemea kwa kuwa kukua kwa mpira wa Tanzania, suala la haki linatakiwa
kuchukua nafasi kubwa sana.
Binafsi
ninapinga kama kweli kuna waamuzi wana mawazo au nia ya kutaka
kuipendelea timu fulani ambalo si jambo sahihi na halina msaada hata
kidogo kwa maisha ya ukuaji wa mpira wa Tanzania.
Pamoja na hivyo, nataka kuwaasa wale ambao wamekuwa bendera fuata upepo, wanalibeba suala hili bila ya kuliangalia kwa kina.
Simba ambayo sasa imefunga mabao 40 katika mechi 17, imependelewa mangapi ambayo wanaweza wakayaelezea na kuwaaminisha watu.
Tumeona
waamuzi hawa wanakosea katika mechi hata zinazoihusisha Yanga na timu
nyingine na si Simba tu, tumeona wanakosea hata katika mechi za Azam FC
au za timu nyingine na wachezaji au viongozi wa timu za Ligi Kuu Bara
wanalijua hili.
Simba
imefunga mabao 40, ukiangalia Yanga wamefunga 20, baada ya bao la jana
dhidi ya Mtibwa Sugar, Lipuli wana mabao 23, Azam FC yenye 22. Tuambiwe
kwa takwimu Simba kapendelewa mara ngapi badala ya hadithi tu.
Kwangu
suala la Simba kapendelewa kama hakuna takwimu basi inakuwa ni
kubabaisha tu mambo na kutaka kuhamisha hoja ya msingi ambayo tunapaswa
kuizungumza.
Mimi nimesema waamuzi wanakosea katika mechi nyingi hata zile ambazo haziihusishi Simba na tunaona.
Maana
yake hapa, hoja ya msingi ni suala la waamuzi kuwa na kiwango duni
katika utekelezaji wa kazi zao na hapa ndipo tunapaswa kupashikilia kwa
ajili ya mpira wa Tanzania.
Tupunguze
ushabiki katika mambo ya msingi, kila mara nimekuwa nikisema hakuna
timu inayomiliki waamuzi na wanapokuwa wanavurunda, sote tunafahamu wapi
pa kwenda na kuwakumbusha kuwa mambo yanaharibika.
Kuendelea
kulia Simba inapendelewa wakati waamuzi wanakosea, ni kufunika makosa
yao kupitia ushabiki, huenda kutengeneza hisia za wengine pia
kupendelewa ili tuwe na ligi ya wanaopendelewa tu, jambo litatufanya
tuwe na akili za hovyo kabisa.
Waamuzi
wanavurunda na hili ndilo suala linatakiwa kufanyiwa kazi, wapate
maonyo au kuchukuliwa hatua kali kwa wale wote wanaoboronga.
Unaona
mechi ya watani Yanga na Simba, bila ya ubishi, ilionekana penalti
waliyopewa Simba ina utata na kweli haikuwa penalti na hili ni kosa la
‘assistant line two’. Bao la pili la Yanga nalo lilikuwa na makosa
sahihi kusema si bao kwa kuwa Mohamed Issa Banka alimsukuma kabisa
Mohamed Hussein Zimbwe aliyejifunga lakini ‘assistant line two’ huyohuyo
akajikausha ili kufunika kosa la kwanza kwa ‘kubalansi’.
Hii
maana yake, hawa waamuzi wanajua matatizo yao na wanachokosea. Hivyo
tusiwape nafasi kabisa ya kuendelea kurekebisha makosa yao kupitia
makosa, wataziumiza timu.
Maana
timu moja itaumizwa kwa makosa na udhaifu wa ubora wa mwamuzi halafu
yeye atajirekebisha kwa kuiumiza nyingine tena, hii si sahihi.
Kwa
sasa si nani anapendelewa kwa kuwa tukiangalia hivyo, hata wale
wanaolalamika wanaweza kukuta timu yao imependelewa zaidi kwa udhaifu wa
waamuzi au makusudi.
Hivyo vizuri kudhibiti pale yanapoanza kutokea maji kuliko kusubiri yatoke halafu tuanze kuchota kuyapunguza.
SOURCE: CHAMPIONI
Post a Comment