Mabingwa watetezi wa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wapo katika presha kubwa ya kutetea taji hilo kutokana na wapinzani wao, Azam FC na Yanga kuwasogelea kwa karibu.
Simba wanaofukuzia taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo ndio vinara wa ligi hiyo hivi sasa wakiwa na pointi 53, katika michezo 21 waliyocheza sawa na Azam FC iliyopo nafasi ya pili ikiwa na pointi 44.
Yanga inashika nafasi ya tatu kwa pointi 38 lakini ikiwa nyuma kwa mechi mbili za viporo ili kufikia idadi ya mechi za Azam na Simba. Endapo Yanga itacheza na kushinda mechi zake mbili za viporo, itafikisha pointi 44 ambazo ni sawa na Azam, hivyo watakuwa wanatofautiana na vinara Simba kwa pointi tisa sawa na mechi tatu, hivyo jambo hilo ni kama linatoa presha kwa Simba.
Vinara hao walianza ligi wakiwa katika ubora wa hali ya juu, lakini katika mechi tatu zilizopita dhidi ya Polisi Tanzania, JKT Tanzania na Namungo walionekana kushuka kiwango kabla ya kurejea tena kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar kwa kasi baada ya kushinda 3-0.
Yanga ilianza vibaya ligi ila kwa sasa inaonekana kuwa katika kiwango bora ingawa bado matokeo yake yanasuasua kutokana na upinzani na Azam FC pia kuna wakati iliyumba kidogo, lakini sasa inarudi katika ubora.
Si kwa wekundu hao tu walio kwenye presha, bali hata wapinzani wake kwa maana ya Yanga na Azam hawawezi kuwa salama katika nafasi zao kutokana na utofauti mdogo wa pointi kutoka kwa wengine walioko nyuma yao.
Timu zinazokuja kwa kasi ni Namungo inayoshika nafasi ya nne kwa pointi 36, Kagera pointi 34 sawa na Coastal pia, ni lazima Yanga na Azam zitakuwa zinacheza kwa presha ya kutafuta matokeo mazuri zikijua wazi kuwa zikipoteza zitakuwa kwenye wakati mgumu.
Bado timu nyingi zina nafasi kuingia nafasi za juu kama zitaendelea kuonesha ushindani katika michezo ijayo kama JKT Tanzania yenye pointi 31, Lipuli 29, Biashara 28, Ruvu 26, Tanzania Prisons 25 sawa na Alliance na Mtibwa 23.
Kuna ambazo ziko hatarini zitakuwa kwenye presha ya kujinasua mapema zisije kuingia kwenye hatari ya kushuka daraja kama KMC pointi 20, Ndanda yenye pointi 19, Mbao 19, Mwadui 18, Mbeya City 18 na Singida United 11, ambao wako mkiani kabisa. Taswira ya msimamo inaweza kubadilika kutegemea na matokeo ya mechi zijazo, hasa kuanzia nafasi ya tatu kushuka chini
Post a Comment