USHINDANI wa Ligi Kuu Bara unazidi kushika kasi ndani ya ardhi ya Bongo kutokana na timu nyingi kutafuta kile ambacho kipo kwenye malengo yao ambayo wamejiwekea.

Tunaona kwamba kwa sasa kila timu inakuja na  mpango wake ambao unawapa matokeo chanya na wapo wale ambao wanajikongoja taratibu.

Singida United mambo bado sio mambo kwani tangu msimu kuanza mwendo wao ni wa kinyonga hawana habari kabisa na ushindani uliopo kwa sasa.

Ninaamini kwamba huenda kuna tatizo ambalo linawakabili hawa ndugu zetu ila inashindwa kuweka wazi katika haya kutokana na kushindwa kufurukuta kwenye mechi zake nyingi ambazo wamecheza.

Ukiachana na Singida United pia hata Ndanda FC, Mbeya City na KMC hizi msimu huu kwa mzunguko wa kwanza mambo kwao yamekuwa magumu.

Kuna umuhimu wa benchi la ufundi kukaa chini na kutazama namna gani wanaweza kuongeza ukali kwenye safu zao za ushambuliaji na kuongeza umakini kwenye safu ya ulinzi.

Ukweli haujifichi kwa timu ambayo itapambana ina nafasi ya kupenya na kubaki ndani ya Ligi Kuu Bara pale ligi itakapomeguka jumla.

Kwa zile ambazo zitakuwa na mwendo uleule itakuwa ni hekaya za Abunuwasi kuziona zikishiriki ligi msimu ujao wa mwaka 2020/21.

Nina amini kwamba kwa kuwa msimu huu timu 16 ndizo zinahitajika kushiriki ligi ina maana kwamba ni timu nne zinashuka daraja moja kwa moja na nyingine mbili zitacheza playoff.

Mtego huu uliotegwa ndani ya ligi muda wake wa kuteguliwa ni sasa. Wachezaji na makocha kazi kubwa kwa sasa ni kuona kwenye mzunguko wa pili kipi kitafanyika.

Ukiachana na suala la kushuka daraja, kuna ishu ya waamuzi kuendelea kupewa mzigo wa lawama kutokana na maamuzi ambayo wanayafanya ndani ya uwanja.

Kuna jambo la msingi na la lazima linatakiwa lifanyike kwa waamuzi ili kufunga mirija yote ya makosa inapotokea kwa sasa na kuongeza utamu wa ligi.

Imekuwa ikielezwa kuwa waamuzi wanadai fedha zao za muda mrefu ambazo hawajapewa kutokana na kazi yao katika hili kuna umuhimu wa kulifanyia kazi hasa kwa mamlaka husika.

Mpira ukiwa na malalamiko mengi unaboa na utapoteza mvuto kwa mashabiki kushindwa kujitokeza uwanjani kutokana na malalamiko haya kuzidi.

Awali tatizo kubwa ilikua kwenye usalama wa mashabiki ambao walikuwa wakipigwa na watu wa usalama nayo ilichangia kupunguza mashabiki ndani ya uwanja mwisho wa siku mambo yakaanza kubadilika linaibuka suala lingine.

Waamuzi ni mhimili wa mafanikio ya soka, jambo moja la msingi wanapaswa walifanye ni kwenda na spidi ya mpira pamoja na kutoa maamuzi sahihi.

Kinachotakiwa kufanyika ni kufuata sheria 17 za mpira ili kuongeza ushindani na kumpata mshindi wa halali ndani ya dakika tisini

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.