IKWIRIRI yenye maskani yake Kibaha, mkoan Pwani ilikuwa timu yake ya kwanza kuanza kuichezea kwenye maisha yake ya soka na sasa amekuwa mchezaji anayekimbiza mafanikio kwa kasi.
Jina lake anaitwa Yusuph Mhilu, nyota anayekipiga Kagera Sugar kwa mkopo akitokea Yanga ambayo iliibua kipaji chake kutoka timu ya Sifa United ya Manzese Dar.
Nafasi yake anayocheza ni mshambuliaji, timu yake imefunga jumla ya mabao 25 amehusika kwenye jumla ya mabao 9 alifunga mabao 7 na pasi mbili za mabao.
Ni mabao matano ameachwa na mfungaji kinara, Meddie Kagere raia wa Rwanda, anayekipiga Simba na anashikilia tuzo ya ufungaji bora kwa msimu uliopita baada ya kufunga mabao 23, Mhilu ni mzawa anayemfukuza taratibu.
Nyota huyo amefunguka mengi anayofikiria kwa sasa, huyu hapa anaanza:-
“Ukizungumzia timu ambazo nimezipitia huwezi kuiacha Yanga kwa kuwa wao walinitoa kutoka timu yangu ya zamani ya Sifa FC ya Manzese na kunipeleka kwenye ile Yanga B, hapo nilipambana na nikapata nafasi ya kucheza timu ya wakubwa pia.
Ilikuaje ukasepa Yanga?
“Wakati huo nilikuwa chini ya Mwinyi Zahera aliniambia kwamba ninaweza kuwa mchezaji mzuri ila kwa Yanga sina nafasi ya kucheza ili niendelee kuonekana ilikuwa ni lazima nitoke nikakubali kuondoka na sasa nipo Kagera na maisha yanaendelea.
Tofauti ya Yanga na Kagera ipo wapi?
“Hapana tofauti kubwa zaidi ya majina tu, kule Yanga ushindani wa namba ulikuwa ni mkubwa na wakati mwingine nilikuwa sipati nafasi ila huku Kagera nina nafasi na ninaonyesha ule uwezo wangu.
Wakati wa dirisha dogo kulikuwa na taarifa za kurudi Yanga ilikuaje?
“Kweli nami niliskia taarifa hizo ila ilikuwa ni presha ya mashabiki. Kwenye timu zetu hapa mashabiki nao wana nguvu, wanakuwa na chaguo lao na mwalimu pia ana chaguo lake niliambiwa kwamba bado nafasi yangu haipo ndani ya Yanga ndio maana nipo mpaka sasa nipo Kagera Sugar. 
Maisha ndani ya Kagera yapoje?
“Tunapambana na tunaishi vizuri, kila mmoja anatoa ushirikiano kwa mwenzake ndio maana tunapata matokeo na kufurahi kwa pamoja. Wakati mwingine tunapoteza na bado tunafurahi pamoja.
Uliifunga Yanga ulikuwa katika wakati gani?
“Hakuna namna nyingine ambayo nilipaswa kuifanya, kazi yangu nikiwa uwanjani sina habari za kuhofia zaidi ni kutimiza majukumu yangu. Mimi ni mshambuliaji nimepewa jukumu la kufunga na nilipofunga maana yake nimetimiza kazi yangu. Ugonjwa wangu ni kufunga na ninapenda kufunga ili kuwa na mabao mengi zaidi.
Mabao mangapi unahitaji kufunga?
“Kufunga napenda siwezi kusema nataka kufunga mabao mangapi ila ninapenda kufunga. Nikiwa uwanjani akili zangu ni kufunga ninafurahi kumuona mlinda mlango akirudi nyavuni na kuokota mpira wangu hiyo safi kwangu.
Mipira mingapi umejikusanyia kwa kufunga?
“Kwenye maisha yangu ya soka mpaka sasa nina mpira mmoja tu, maana kule kwenye timu za mtaani hakuna ambaye alikuwa anajali unaweza kufunga mibao kibao ila hakuna anayeweza kukupa mpira. Nilifunga hat trick kwenye mechi ya kombe la Shirikisho.
“Tulicheza na Rufiji United tulishinda mabao 4-1, hapo ndo nikasepa na mpira nina imani mingine inakuja.
Mabao unayofunga unatafuta nini?
“Ushindi kwa timu kwanza, ila hata ufungaji bora. ni kitu kizuri nahitaji pia kutwaa tuzo hiyo
Mafanikio yako yanabebwa na nini?
“Kujituma na kufuata maelekezo ya mwalimu kwa kile ambacho ananiambia. Ushirikiano ambao ninaupata ndani ya timu unanibeba pia.
“Muhimu kumtanguliza Mungu katika kila jambo na mafanikio yanakuja bila kusahau juhudi.
Miaka mitano unajiona wapi?
“Jambo la kuomba uzima kwa Mungu, ninaamini kwamba nitatimiza ndoto yangu ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Beki yupi unadhani ni mgumu uwanjani?
“Wapo wengi na inategemea wakati mwingine yupoje, Pascal Wawa wa Simba ni miongoni mwa mabeki wazuri uwanjani. Anatumia nguvu kidogo na akili nyingi muda mwingine vyote.
Nje unamtazama nani ?
“Raheem Sterilng wa Manchester City ananifanya nijifunze vingi. Kuanzia spidi, juhudi ndani ya Uwanja kwa kila anachokifanya ninapenda kujifunza.
Ligi kiujumla unaitazamaje?
“Ligi ya msimu huu sio poa maana kila siku ushindani ni mkubwa na kila timu inapambana.Hali hiyo inatufanya tuzidi kupambana kupata matokeo mazuri mashabiki watupe sapoti,” anamalizia Mhilu.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.