MOTO wa Ligi Kuu Bara unazidi kufukuta kwa kasi jambo ambalo linafurahisha kwa kila mmoja kufuatilia kwa ukaribu na kuona namna gani timu yake inaweza kupata matokeo kwenye mechi zake.
Kila mmoja anapambana kupata kile ambacho anakipanda kwani matokeo mazuri uwanjani hayaji kwa maajabu zaidi ni kujipanga na kupambana kutafuta pointi tatu.
Wachezaji jukumu lenu ni moja tu ndani ya uwanja kucheza kwa juhudi kutafuta ushindi kwa timu ambayo inakulipa mshahara na ni kazi yako kuonyesha uwezo wako.
Tunaona ushindani unazidi kupamba moto kila inapoitwa leo kutokana na kila timu kutafuta kupata matokeo mazuri ndani ya uwanja hili ni jambo la msingi.
Kila mmoja anahitaji kupata pointi tatu kwani hakuna timu inayoingia uwanjani ikiwa inafikiria kushindwa ama kufungwa kutokana na maandalizi ambayo wameyafanya.
Jambo moja ambalo linavutia ni kwamba ushindani umekuwa mkubwa kwa timu zote kwa yule ambaye atazubaa kwa mwendo huu asishangae akiachwa nyuma na wengine wakisonga mbele.
Mzunguko wa kwanza kwa sasa umebakiza mechi kadhaa kwa baadhi ya timu ambapo inaaminika kwamba kabla mwezi huu Februari haujameguka timu zote zitakuwa zimeanza safari nyingine kwenye mzunguko wa pili.
Mzunguko wa kwanza unaisha huku kukiwa na mambo kadha wa kadha ambayo yametokea na yameacha rekodi kwa wachezaji na makocha pia.
Tumeona mashabiki wakijotokeza kwa wingi kwenye mechi za hivi karibuni inatia moyo na inaongeza morali kwa mashabiki kupambana kupata matokeo wakiwa ndani ya uwanja.
Mashabiki wamekuwa ni chachu ya kufikia mafanikio kwa wachezaji ambapo wamekuwa wakipambana kutafuta matokeo mazuri muda wote.
Kikubwa ambacho mashabiki wanakihitaji ni kuona timu zao zinashinda na wachezaji wanacheza kwa kujituma muda wote bila kuchoka.
Ukweli usiopingika ni kwamba matokeo mabaya yanawaumiza mashabiki ambao wanapenda kuona wanapata burudani na soka la kwenye kitabu jambo litakalofungua njia ya wachezaji kupata nafasi ya kucheza nje ya nchi.
Malengo makubwa ya timu ni kuona inapata ushindi kwenye mechi wanazocheza na kufungua wigo mpana wa mashabiki kuendelea kujitokeza kwa wingi ndani uwanjani.
Kumekuwa na mapungufu ambayo yanaonekana na kumaliza ile ladha ya soka ni suala la waamuzi kuwa na kasi ya kutoa maamuzi ambayo muda mwingine yanaumiza upande mmoja na kuupa faida upande mwingine.
Sekta ya uamuzi imekuwa ikielemewa na sehemu moja muhimu ambayo ni ile ya kutafsiri sheria ya kuotea ambayo ikitafsiriwa vizuri ni maumivu kwa timu iliyokuwa ipo kwenye nafasi na faida kwa timu iliyokuwa kwenye wakati mgumu.
Pia muda mwingine imekuwa haina matokeo chanya kwa wanaofanyiwa ama kutokufanyiwa kutokana na matokeo yaliyopo ila bado inabaki kutoa maumivu.
Ukitazama kwenye mechi za hivi karibuni kumekuwa na mkanganyiko kwenye sheria hii ambayo ni ngumu kwa wengi kwenda nayo sawa kwa sasa ndani ya ligi.
Ukweli ni kwamba maisha ya soka yamebadilika na mpira umekuwa na kasi na wachezaji nao wanacheza kwa kasi isiyo ya kawaida jambo ambalo linawafanya washindwe kutoa maamuzi kwa haraka.
Spidi ya mpira imekuwa kubwa kuliko ile ya wamuzi ni sababu inayofanya muda mwingine washindwe kufanya kile ambacho wengine wanakiona wakiwa nje ya Uwanja.
Pia ni kwamba suala la kuotea linahitaji jicho la pili kulitazama na kulitolea maamuzi ndani ya uwanja kwa wakati sahihi jambo ambalo linafanya kila siku kuwe na kelele kwamba timu moja inapendelewa.
Hebu tazama wakati Simba inashinda mabao 3-2 mbele ya Namungo mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa ulikuwa ni mzuri na ushindani ulikuwa mkubwa ila bao la mwisho la Meddie Kagere wengi wanadai ni la kuotea.
Pia bao hilo lietoa adhabu kwa mshika kindera kwa kufungiwa miaka mitatu kuchezesha soka ndani ya Bongo jambo ambalo linaonesha kuna tatizo kwenye maamuzi.
Achana na hilo bao baada ya Simba kuonekana wamependelewa kwenye mechi yao mbele ya Namungo mchezo wao unaofuata mbele ya Coastal Union mambo yakawa tofauti.
Mshambuliaji yuleyule alifunga bao lilikataliwa na ikaelezwa kwamba aliotea jambo ambalo ni gumu kuamini limetokea na jambo hili pia linaumiza.
Mechi nyingine kwa Simba ilikuwa ni ya Kombe la Shirikisho mbele ya Mwadui ambapo Simba ilishinda mabao 2-1 bado kulikuwa na malalamiko yaleyale kwa upande wa waamuzi kutafsiri sheria ya kuotea.
Hili suala linapaswa litazamwe kwa umakini mkubwa na kutafuta njia bora ya kutatua hili tatizo ili kuendeleza utamu wa ligi ambayo inazidi kukata mbunga
Hata kwenye mchezo wa Yanga na Mtibwa Sugar bado kulikuwa na tatizo aina hii ambapo iliamuliwa nafasi ya kuotea kwa mchezaji wa Mtibwa Sugar jambo ambalo limebaki likijadiliwa kwenye mitandao na vijiweni.
Kwenye mchezo wa yanga dhidi ya Coastal Union, mchezaji wa Yanga alichezewa faulo ndani ya 18 ikawa kona bao kuna tatizo inabidi lifanyiwe kazi katika hili.
Hakuna sheria ambayo imewekwa na inavunjwa makusudi na wale wanaoamua namna gani sheria iende hasa ndani ya sheria 17 za mpira.
Ugumu huu haupo ndani ya Ligi Kuu Bara Bongo pekee bali hata nje ya nchi kuna tatizo hili pia la sheria ya kuotea nafasi ya kufunga ama kufungwa.
Wenzetu England wamepasua kichwa kutafakari jibu la hili tatizo wakaamua kuja na VAR ili kulipunguza suala hili lakini bado malalamiko yapo na yanaendelea kwenye sheria hii.
Kama itawezekana ni wakati wa kutafuta mbadala wa suala hili ndani ya Bongo ikiwezekana iletwe tekonolojia ya VAR ili kupunguza malalamiko na kuondoa kelele ambazo zinakuwa zinaendelea.
Ikiwa itakuwa ngumu kuna umuhimu wa kuongeza mwamuzi mwingine ambaye atakuwa nyuma ya goli ili kupunguza kasi ya mpira akiwa karibu na kuongeza umakini.
Huenda itasaidia kwetu na kuongeza nguvu kwenye soka letu ambalo linazidi kukua ila malalamiko ya waamuzi yamekuwa mengi kila iitwapo leo.
Ugumu wa ligi unatokana na ushindani uliopo pale ambapo wengi wanatazama sehemu ya kutokea ili kupunguza maumivu ya kupoteza ama kupotezwa
Post a Comment