Na Saleh Ally
MTANZANIA Mbwana Samatta amefanikiwa kucheza mechi mbili tu katika kikosi cha Aston Villa ya England lakini tayari ni maarufu sana.


Samatta amecheza mechi moja ya Carabao Cup dhidi ya Leicester City na wamefanikiwa kufika fainali, sasa watakutana na Manchester City jambo linalosubiriwa kwa hamu sana.


Mechi ya pili ilikuwa ni ya Premier LEague, Samatta akiweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza ligi hiyo. Kama haitoshi, katika mechi ya kwanza akafanikiwa kufunga bao lake la kwanza licha ya kuwa walipoteza kwa mabao 2-1.


Mambo haya yamechangia kumfanya awe maarufu kwa mashabiki wa Aston Villa ingawa lile la mashabiki wengi wa Tanzania kuvamia mitandao nalo lilichangia.


Kuendelea kuifahamu vizuri Aston Villa ambayo yuko Samatta ni vizuri zaidi na mmiliki wake, anatokea Afrika kwa maana ya nchini Misri.


Nassef Sawiris ndiye tunayemzungumzia. Mmiliki wa timu hiyo ya England ambayo ni moja ya timu kongwe katika soka la England.


Ingawa si maarufu sana Tanzania, nchi nyingi duniani amekuwa maarufu kutokana na utajiri wake pia akijihusisha na mambo kadhaa yakiwemo ya michezo.


Unapowataja watu kadhaa maarufu hasa matajiri katika soka kama Roman Abramovich, mmiliki wa Chelsea au Sheikh Mansour anayeimiliki Manchester City, karibu kila mpenda soka anawafahamu lakini kwa Tanzania Sawiris si sana.


Pamoja na hivyo, katika orodha ya matajiri wanaomiliki timu za England, kwa utajiri Sawiris anashika namba tano baada ya Sheikh Mansour anayeongoza akiwa na utajiri wa dola bilioni 30 akitokea katika familia ya kifalme ya Abu Dhabi.


Abramovich anafuatia akiwa na dola bilioni 12.4, nafasi ya tatu ni mmiliki wa Arsenal FC, huyu ni Mmarekani Stan Kroenke mwenye utajiri wa dola bilioni 8.7 na nafasi ya nne ni mmiliki wa Klabu ya Wolverhampton, anaitwa Guo Guangchang, utajiri wake ni dola bilioni 6.7.


Sawiris mwenye utajiri wa dola bilioni 6.4, anafunga tano bora ya matajiri wanaomiliki timu za Ligi Kuu England kwa maana ya utajiri wao.


Wakati Sheikh Mansouri ana rekodi ya utajiri ya dola milioni 82.7 kumsajili Kevin De Bruyne kutoka Wolfsburg, Sawiris naye amejitutumua kwa kuwa na rekodi ya kutoa dola milioni 27.2 kumsajili Wesley kutoka Club Brugge ya Ubelgiji. Mshambuliaji huyu ndiye aliyeumia na kusababisha Samatta kutua Genk.


Sawiris ni namba nne kwa utajiri barani Afrika akiwa ametokea katika familia ya Onsi Sawiris, yeye akiwa ni mtoto wa  mwisho katika watoto watatu. Kaka zake wawili ni Naguib na Samih.


Utajiri wa Sawiris ni pauni bilioni 7.5 na inaonekana alianza kupambana na biashara akiwa chini ya baba yake mzazi kuanzia mwaka 1982 kupitia kampuni ya ujenzi ya Orascom Construction na mwaka 1995 akakabidhiwa mikoba kuwa CEO na juhudi zake kubwa na ubunifu uliifanya kampuni hiyo kukua kwa kasi kubwa.


Kadiri siku zinavyosonga alizidi kujitanua kimasoko na kufikia kufungua baadhi ya makampuni kadhaa Dubai ambayo yalizidi kumuongezea utajiri.


Sawiris alizidi kujitanua katika biashara mbalimbali ukiachana na zile za ujenzi lakini nyingine zilizojihusisha na michezo, mwaka 2015 kupitia kampuni yake ya NNS Holding Sarl ya nchini Luxembourg alinunua baadhi ya shea zilizoiwezesha kampuni hiyo kusimamia baadhi ya kazi za kampuni kubwa ya michezo ya Adidas.


Julai mwaka 2018, ikatangazwa kwamba Sawiris atakuwa ndiye Mwenyekiti wa Klabu ya Aston Villa ya England akichukua nafasi ya aliyekuwa mwenyekiti, Tony Pia.


Sawiris alichukua nafasi ya uenyekiti baada ya kununua hisa za kiwango cha 55% zikiwa chini ya Kampuni ya NSWE ambayo inaendeshwa na kampuni yake kubwa ya NNS inayoshirikiana na bilionea mwingine wa Kimarekani Wes Edens.


Wakati Forbes ilimtangaza mwaka jana kuwa tajiri namba nne barani Afrika, kuna taarifa nyingine zimeeleza Sawiris amekuwa akikua haraka sana kiuchumi.


Kaka yake mmoja, Naguib Sawiris pia ni mmoja wa matajiri, akanadiriwa kuwa na utajiri wa dola milioni 2.9, na hii inawafanya kuwa familia tajiri zaidi nchini Misri.

Kampuni ya Orascom Telecom ya Sawiris imewekeza hadi nje ya Misri katika masuala ya mawasiliano na zaidi ni katika nchi za  Lebanon na Pakistan.


Sawiris pia anamiliki kampuni kubwa ya mawasiliano ya Koryolink ambayo ni kampuni ya mtandao wa simu kwa mfumo wa 3G nchini Korea Kaskazini.


Mwaka 2015, Sawiris alizidi kuwa gumzo zaidi duniani baada ya uamuzi wake wa kununua kisiwa kilicho katikati ya Ugiriki na Italia kwa ajili ya kujenga makazi ya wakimbizi ambao wengi wao wamekuwa wakivuka kutoka Afrika kwenda Ulaya kupitia bahari ya Mediterranean na bahati mbaya wengi wao wamekuwa wakifa maji.


Suala la kuwa na watu karibu milioni 6 wanaomfuatilia katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter umemfanya pia kuwa mmoja wa watu maarufu zaidi duniani.


Hii inatoa nafasi kwa Watanzania kuona kuwa Samatta analazimika kuwa katika presha kama mchezaji kwa kuwa anatambua ana deni kubwa.


Deni litaanzia kwa kocha akimtaka kuona anafanya vizuri, lakini kuna presha ya mashabiki ambalo hili ni jambo la kawaida.


Kwa Samatta kwa kuwa ameshacheza Ulaya kwa zaidi ya misimu miwili, anaelewa hata presha ya wamiliki kama Sawiris ambaye lazima atakuwa anataka kupata mafanikio.


Hawezi kuwa anaingilia uchezaji wa timu au vinginevyo lakini mwisho wa msimu atataka kuona kikosi kimefanya vema zaidi.


Ndiyo maana kocha kama Dean Smith anapoona kuna namna ya kujiokoa anaweza kumshawishi mmiliki kama Sawiris kutoa fedha takribani pauni milioni 10 kumpata mchezaji kama Samatta akiamini atakuwa jibu la matatizo yake ya ushambulizi.


Mabilioni huwekeza katika mpira kwa sababu ya biashara lakini wako huwekeza sababu ya mapenzi yao kwa mchezo huo ingawa kamwe hawakubali kupata hasara kutokana na wanachokiwekeza. Huyu, ndiye bosi mpya bilionea wa Samatta

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.