LICHA ya Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, kuweka wazi kwamba chanzo cha kupoteza juzi ni kutokana na wapinzani wao kuwa wazuri eneo la katikati, Mbelgiji wa Simba, Sven Vandenbroeck amekiri washambuliaji wawili mbele walichangia ushindi wao wa mabao 3-0 pamoja na ari kubwa kutoka kwa kikosi kizima.

Sven kwa muda mrefu amekuwa akilalamikiwa na mashabiki wa timu hiyo kwa kukumbatia mfumo wake wa mshambuliaji mmoja mbele, jambo ambalo wanadai linatoa nafasi kwa mabeki wa timu pinzani kucheza kwa uhuru zaidi na kuwapa mwanya wa kusukuma mashambulizi mbele.

Hata hivyo, kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa JKT Tanzania Ijumaa iliyopita, kilimuamsha Sven na juzi dhidi ya Mtibwa kulazimika kuanza na washambuliaji wawili mbele, Meddie Kagere na John Bocco, hatua iliyosaidia kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza 1-0.

Bao hilo likifungwa na Bocco kwa ushirikiano mzuri na Kagere na kiungo Clatous Chama kabla ya kipindi cha pili Mohamed Hussen 'Tshabalala' na Hassan Dilunga 'HD' kuongeza mawili, hivyo kushinda kwa 3-0.

Baada ya mechi hiyo, Katwila alisema wapinzani wao walikuwa bora zaidi eneo la katikati, hivyo kuharibu mipango yao na kisha kutumia mwanya huo kusukuma mashambulizi mbele na kufanikiwa kuwaadhibu.

"Simba walikuwa bora zaidi katikati, jambo lililoharibu mipango yetu na kusababisha kushambuliwa zaidi, nimeyaona makosa yaliyofanyika na nitakwenda kuyafanyia kazi kabla ya mechi ijayo dhidi ya JKT Tanzania]," alisema.

Lakini Sven licha ya kuwapongeza wachezaji wake kwa ari kubwa ya ushindi waliyoionyesha mwanzo mwisho wa mchezo huo wa juzi, Nipashe lilipomuuliza anauonaje mfumo wa washambuliaji wawili mbele alikiri kufanya kazi vizuri.

"Ni kweli wamecheza vizuri na umeonekana kutupa matokeo, lakini kwa ujumla timu nzima imecheza vizuri na wachezaji walikuwa na ari ya ushindi mwanzo mwisho wa mchezo.

"Itakapolazimu tutakuwa tukibadilisha mfumo kutokana na aina ya mechi na ninatumai ari hii kwa wachezaji itaendelea pia katika mechi nyingine," alisema kocha huyo aliyerithi mikoba ya Mbelgiji mwenzake, Patrick Aussems huku akiongeza.

"Kwa ujumla matokeo mazuri ni kitu tulichokuwa tunakihitaji, hata wachezaji pia walikuwa wanalitambua hilo, kujituma kwao na juhudi zao ndio mafanikio yetu."

Simba ambayo imeshuka dimbani mara 21 hadi sasa ikiwa kileleni na alama 53, Jumamosi itakuwa ugenini katika Uwanja wa Samora kuvaana na Lipuli FC iliyopo nafasi ya tisa na alama zake 29 baada ya kucheza idadi ya mechi kama hizo za mabingwa hao watetezi

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.