Kikosi cha Simba kilitua juzi Alhamisi katika ardhi ya Iringa tayari kwa mchezo wao wa kesho Jumamosi dhidi ya Lipuli FC, ambapo kocha wa wenyeji hao, Julio Elieza amekiri kuwa Simba ipo katika kiwango bora kwa sasa.

Simba walitua mchana wakitokea mkoani Morogoro walipocheza mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar na kushinda 3-0, Jumanne ya wiki hii ambapo sasa watakuwa na kibarua kingine cha kutafuta alama tatu dhidi ya Lipuli katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Samora.

Simba wapo kileleni na pointi zao 53, wakiwa wamecheza michezo 21, huku Azam FC wenye pointi 44 wakiwa katika nafasi ya pili baada ya michezo 21, Yanga wapo katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 38 wakicheza michezo 19, huku Lipuli wenyewe wakishika nafasi ya tisa na pointi 29 baada ya kucheza michezo 21.

Elieza aliliambia Championi Ijumaa kuwa siyo rahisi kwa sasa kupata ushindi mbele ya timu kubwa kama Simba, lakini kwa kuwa soka ni mchezo wa kupambana kutafuta nafasi, watajitahidi kucheza kulingana na maandalizi waliyofanya ili kutafuta pointi tatu dhidi ya wapinzani wao hao ambao ni mabingwa.

“Simba wapo imara sana kwa sasa, siyo rahisi kupata matokeo chanya unapocheza na timu kubwa, lakini hiyo haina maana kuwa tutakubali kufungwa, soka ni mpira wa kutafuta nafasi, tutajitahidi kucheza kulingana na maandalizi tuliyofanya ili kuona tunapata pointi tatu mbele ya Simba katika mchezo wa Jumamosi,” alisema Elieza

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.