UONGOZI wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umemtangaza Almas Kasongo kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu mpya wa Bodi ya Ligi (TPLB) kuchukua nafasi ya Boniface Wambura.

Akizungumza Dar es Salaam jana Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred alisema mchakato wa kumpata Mtendaji Mkuu wa Bodi ya ligi ulifanywa kwa uwazi na kamati inayojitegemea nje ya TFF ili kuondoa makandokando na mchakato ulikwenda vizuri.

“Rais wa TFF katiba ina mamlaka ya kuunda kamati iliyosimamia mchakato kwa weledi hadi Kasongo akapatikana na jina lake kupelekwa kwenye kamati ya utendaji kwa ajili ya kuthibitishwa, Kasongo ni msomi mzuri kwenye masuala ya fedha naamini anafaa kuongoza TPBL,” amesema Kidao.

Kwa maana nyingine Kasongo ambaye alikuwa Ofisa Mwandamizi wa masuala ya biashara wa Shirika la Nyumba pia Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) cheo hicho kimekoma baada ya kutangazwa kuwa Mtendaji wa Bodi.

Baada ya kutangazwa Kasongo msomi mwenye shahada ya Uzamili kutoka London South Bank University cha Uingereza amesema kipaumbele chake ni kwenda kusimamia klabu zote kutekeleza matakwa ya leseni za klabu.

“Katibu hapa amezungumza muda mrefu sana na msingi wa alichozungumza ni leseni za klabu na naamini klabu zikitekeleza matakwa ya leseni za klabu mpira utafanikiwa,” alisema Kasongo.

Pia Kasongo alisema yeye ni mtu sahihi kushika wadhifa huo kwa sababu ana uzoefu katika soka kwa maana ya kucheza na kuongoza katika nyadhifa mbalimbali.

“Niliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha soka wilaya ya Ilala (IDFA) miaka miwili, Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kwa miaka nane na kiongozi wa klabu kwa miaka 15 na kuhudumu katika kamati mbalimbali hivyo uzoefu wa kutosha,” amesema Kasongo

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.