SHIZA Kichuya mzee wa kona bao, ametibua hali ya hewa Simba kutokana na uwezo anaozidi kuonyesha kwenye mazoezi ya timu yake hiyo kiasi cha kuwatisha wachezaji wengine wanaocheza nafasi kama yake. Kichuya amejiunga na Simba kwenye dirisha dogo la msimu huu akitokea Pharco ya Misri ambayo inashiriki Ligi Daraja la Pili nchini humo.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zimeliambia Championi Jumamosi kuwa, tangu aanze kufanya mazoezi na timu hiyo hivi karibuni mambo yamebadilika, kwani wachezaji aliowakuta ambao wanacheza nafasi kama yake wanadaiwa kuingiwa na hofu ya kupoteza namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Hali hiyo inatokana na uwezo mkubwa ambao amekuwa akiuonyesha mazoezini na kumfanya kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck kuonekana kuvutiwa naye. Wachezaji ambao Kichuya anacheza nao namba moja ni Francis Kahata, Deo Kanda Ibrahimu Ajibu na Hassan Dilunga.
“Wachezaji hawa mara kwa mara ndiyo wamekuwa wakiachiana nafasi ya kucheza, kwa hiyo kitendo cha Kichuya kuja na kuonyesha uwezo mkubwa mazoezi kimewafanya wawe na hofu ya kupoteza nafasi kwani hata kocha ameshamuelewa.
“Kichuya ana uwezo wa kucheza winga zote za kulia na kushoto kwa hiyo hilo ndilo limekuwa likiwafanya wachezaji hao waingiwe na hofu,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Hata hivyo, hivi karibuni Vandenbroeck aliliambia gazeti hili kuwa: “Katika kikosi changu siangalii jina la mtu ila uwezo, mchezaji yeyote atakayekuwa anafanya vizuri mazoezini ndiye atakuwa akipata nafasi ya kucheza.”
Post a Comment