NA SALEH ALLY
MBWANA Ally Samatta ametua England na kujiunga na Aston Villa ambayo iko katika harakati za kupambana kuhakikisha inatoka kwenye janga la kuteremka daraja.
Nafasi ya kujiokoa ipo lakini haiwezi kuwa nyepesi na inahitaji mapambano hasa kuhakikisha wanaondoka walipo kwa sasa.
Vita, kawaida inahitaji askari imara, Samatta amekuwa sehemu ya nyongeza ya askari anayeaminika kuwa ni bora lakini ili mambo yawe vizuri lazima kuunganisha vizuri nguvu mpya na iliyokuwepo.
Kikosi cha Aston Villa baada ya mechi 24, bado hakijawa imara sana kujiweka katika nafasi ambayo inaweza kuonekana ni sahihi kwa kipindi husika kwa maana ya kushika Top Four au nafasi ya kucheza Kombe la Europa League.
Hata hivyo, inaonekana kuna uwezekano mkubwa kama timu hiyo angalau itapata ushindi kwa asilimia 75 ya mechi zake zilizobaki za Ligi Kuu England, inaweza kutoka chini kwa maana ya mkiani na kuwa moja ya timu zinazowania kucheza Europa League na kuwa na uhakika wa kutoteremka.
Kitakwimu bado hawajawa vizuri sana lakini unaona kuna mwelekeo kwa kuwa Aston Villa wamepiga mashuti 105 yaliyolenga lango na kuwa sehemu ya baadhi ya timu zilizofanya vema kwa kiwango cha kati, lazima waboreshe.
Unaona ukijulimsha mashuti ambayo pia hayakulenga lango, jumla ni 151 ambayo ni ya mguu wa kulia na 95 kutoka mguu wa kushoto.
Wastani wa takwimu si mzuri kwa Aston Villa kwa kuwa wamefunga mabao 31 na kufungwa 45, hivyo kutengeneza GD ya -14, jambo ambalo si zuri kwa timu inayopigania ubora.
Unaona Mbwana Samatta anaingia Villa akiwa sehemu ya tegemeo kubwa la ukombozi kwa maana ya kusaidia mabao mengi ya kufunga yapatikane ili kurekebisha ile hali ya kuwa na mabao machache ya kufunga.
Vyovyote itakavyokuwa, Samatta atalazimika kuunganisha nguvu yake kwa uelewano na msaada wa pamoja na Jack Grealish, ambaye kwa sasa ni Mfalme wa Villa.
Kijana huyo, ndiye tegemeo na mkombozi mkubwa ambaye kama nguvu yake aliyonayo sasa itaungana vizuri na Samatta kama ataweza kuwa na kiwango kizuri, hakuna ubishi wataikomboa kutoka walipo.
Grealish ana umri wa miaka 24, kijana ambaye alizaliwa katika Mji wa Birmingham, eneo wanalotokea Aston Villa. Kwa sasa amekuwa tegemo kubwa katika kikosi cha Dean Smith, si vibaya ukamuita ndiye roho ya timu huyo.
Katika soka, hakuna longolongo kwa kuwa kila kitu ni hesabu na mwisho kinakwenda kwenye takwimu. Kabla ya Samatta kuanza kucheza, Grealish ndiye tegemeo na mfalme wa Aston Villa kwa kipindi hiki.
Grealish ndiye anaongoza kwa mabao ya kufunga akiwa nayo saba na unaona anafuatiwa na Wesley, raia wa Brazil ambaye amekuwa chanzo cha Villa kuhakikisha wanampata Samatta baada ya kuwa ameumia.
Grealish amekuwa akicheza nafasi ya kiungo mshambulizi. Kuumia kwa Wesley, kuliwalazimisha Villa kuanza kumtumia kijana huyo katika nafasi ya Wesley aliyeumia akiwa na mabao matano, sasa Grealish ana saba. Mwingine mwenye mabao mengi ni Anwar El Ghazi mwenye manne.
Ukienda upande wa wenye mchango mkubwa katika pasi za mwisho zilizozaa mabao, yaani asisti, anayeongoza ni Grealish tena. Amepiga asisti tano, maana yake ameshiriki katika mabao 12 ya Aston Villa kwa maana ya aliyofunga na aliyozalisha.
Katika timu mtu anayetengeneza mabao ni muhimu sana kama ilivyo kwa mfungaji. Lakini ukipata mwenye uwezo wa kutengeneza na kufunga, huyu ni muhimu sana, sana.
Upande wa pasi, mwenye pasi nyingi zilizofika alipozipeleka ni Grealish pia. Amepiga pasi 763 katika mechi za Premier League na zimefika. Ndiye mchezaji anaongoza kwa pasi nyingi zaidi katika kikosi hicho akifuatiwa na Tyrone Mings mwenye 698 na Douglas Luiz aliyepiga 535.
Ukirudi kwenye takwimu za waliopiga mashuti mengi kwenye Premier League katika kikosi cha Aston Villa, Grealish ndiye anayeongoza baada ya kupiga mara 46, akifuatiwa na El Ghazi mwenye 40 na nafasi ya tatu ipo kwa John McGinn mwenye 38.
Ukiangalia mwendo wa Grealish maana yake atakuwa msaada mkubwa kwa Samatta, ana uwezo wa kumpa pasi bora zinazofika, anatoa asisti za mabao lakini anafunga pia ambalo ni jukumu la Samatta.
Hivyo, ukiachana na kwamba atatoa pasi nzuri kwa Samatta ifungwe, basi ana nafasi ya kuwachanganya mabeki wakimuona ni hatari sana, halafu Samatta akapata wepesi wa njia ya kufanya yake.
Bado Villa ina watu wengi wanaoweza kuwa msaada kwa kuwa Samatta na Grealish hawawezi kupambana peke yao. Kama wao wanataka kufunga, wako ambao watatoa pasi kuchezesha timu au watapambana kukaba.
Zimbabwe Marvelous Nakamba, Bjon Engels, Matt Targett na McGinn ni kati ya watu wenye uwezo mkubwa wa kuchezesha kikosi lakini bado ilionekana kuna changamoto ya umaliziaji na Samatta anakuwa sehemu ya utatuzi wa tatizo hilo.
Samatta anajulikana katika kulenga lango lakini wachezaji kama Luiz, Trezeguet via McGinn ni hatari katika mashuti au kulenga lango kama ilivyo kwa El Ghazi.
Kocha Dean Smith alichokuwa ameangalia zaidi kama nilivyokueleza awali ni kupata mabao mengi ya kufunga ili kujiimarisha katika upatikanaji wa pointi tatu.
Pamoja na hivyo, unaona Dean amejiimarisha katika suala la mabao mengi ya kufungwa ndiyo maana amemsajili kipa mkongwe, Pepe Reina ambaye alicheza Premier League kwa muda mrefu.
Yeye tayari ameanza kuonyesha cheche katika mechi iliyopita, ikionyesha wazi Dean hakukosea kumrudisha tena England na sasa ni zamu ya Samatta ambaye anasubiriwa kwa hamu kubwa kuingia uwanjani na kuanza kazi iliyompeleka Villa.
TAKWIMU:
MASHUTI
1. Jack Grealish 46
2. Anwar El Ghazi 40
3. John McGinn 38
4. Trezeguet 35
5. Wesley 35
PASI ZILIZOFIKA
1. Jack Grealish 763
2. Tyrone Mings 698
3. Douglas Luiz 535
4. M. Nakamba 499
5. Bjon Engels 448
ASISTI:
1. Jack Grealish 5
2. Anwar El Ghazi 4
3. Frederic Guilbert 2
4. Conor Hourihane 2
5. Ezri Konsa Ngoyo 2
MABAO:
1. Jack Grealish 7
2. Wesley 5
3. Anwar El Ghazi 4
4. Trezeguet 3
5. Conor Hourihane 3
Post a Comment