KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael amesema kuwa tabia ya kuchezea mpira na chenga za maudhi zinazofanywa na Bernard Morrisson raia wa Ghana, hafurahishwi nayo kwani itaigharimu timu yake.
Morrison, amecheza mechi mbili sawa na dakika 180, mechi yake ya kwanza ya ligi dhidi ya Singida United timu yake ilishinda mabao 3-1 alionyesha udambwiudambwi wa kuchezea mpira na kutembea juu ya mpira na alifanya hivyo kwenye mechi ya Shirikisho dhidi ya Tanzania Prisons wakati Yanga ikishinda mabao 2-0.
Eymael amesema kuwa alitumia muda mwingi kuzungumza na Morrison kuhusu tabia yake hiyo na kumweleza wazi anapaswa aiche mara moja kabla haijaigharimu timu.
“Mchezaji mzuri anafanya vitu vizuri uwanjani na kwa vitendo inapofikia hatua anakuwa ni mtu wa kufurahisha mashabiki sio tabia ya nzuri, nilimwambia aache na acheze kwa juhudi kuipa matokeo timu yake hakuna kingine ambacho mashabiki wanahitaji.
“Duniani kote kwa yule ambaye anafuatilia mpira kwa kuzitazama timu kubwa ikiwa ni pamoja na Liverpool, Juventus, Manchester United hakuna anayefanya mambo hayo, kuna Mohamed Salah, Sadio Mane wote wa Liverpool hawafanyi haya mambo ila ni wachezaji wazuri,” alisema Eymael.
Yanga ipo nafasi ya nne kwenye msimamo imecheza jumla ya mechi 15 imejikusanyia pointi 28 na kinara ni Simba mwenye pointi 44 akiwa amecheza mechi 17
Post a Comment