MBELGIJI Sven Vanderboeck ambaye ndiye bosi mkuu wa benchi la ufundi la Simba, ametanabaisha kuwa licha ya kwamba wapo kileleni mwa msimamo wa ligi, lakini ameona kuna ugumu mkubwa katika ligi hiyo huku akipanga kuzicheza mechi zake kiakili.
Mbelgiji huyo ambaye amechukua nafasi ya Patrick Aussems, ameifanya Simba iendelee kukaa kileleni mwa ligi ikiwa na pointi 41 ambazo ni sita mbele ya wapinzani wao Azam FC walio nafasi ya pili.
Kocha huyo ambaye ana miezi miwili tangu atue Tanzania, hadi sasa ameingoza Simba kwenye mechi za ligi dhidi ya Lipuli FC, KMC, Ndanda, Yanga, Mbao na Alliance huku akivuna pointi 16, akishinda mechi tano na sare moja.
Sven ameliambia Spoti Xtra, kwamba anauona ugumu mkubwa kwa sababu kila timu wanayocheza nayo inacheza kwa kujituma kutaka kupata pointi huku pia ugumu wa ratiba ukizidisha ugumu huo. “Unajua wakati nakuja hapa nilifikiri kila kitu kitakuwa rahisi tu lakini nimegundua ni tofauti kabisa.
Ligi ni ngumu sana kwa sababu kila timu ambayo tunacheza nayo inacheza zaidi ya ule uwezo wao kwa ajili ya kutuzuia.
“Lakini pia nimegundua ukicheza na hizi timu ambazo zinaonekana ndogo ushindani huwa mkubwa sana na ndiyo maana kama umeangalia inakuwa hatuna ushindi mkubwa sana kwao, tunashinda kwa mabao machache mno.
Kitu kingine ambacho kinaongeza hali hiyo ni kukosekana kwa mua mrefu wa kupumzika kutokana na ratiba yetu ilivyo,” alimaliza Mbelgiji huyo.
Post a Comment