SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeiagiza Kamati ya Maadili kufuatilia ukweli kuhusu tuhuma za upangaji wa matokeo zilizotolewa na kipa wa Yanga, Ramadhani Kabwili.

Akizungumza Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo amesema baada ya TFF kusikia tuhuma hizo zilizotolewa na Kabwili kupitia vyombo vya habari, sekretarieti imeiandikia barua Kamati yake ya Maadili kufanyia kazi suala hilo.

“TFF itavijulisha vyombo vingine vya usalama ili visaidie uchunguzi na kuchukua hatua stahiki,” alisema Ndimbo.

Kabwili ambaye ni kipa wa tatu Yanga, amenukuliwa na kituo kimoja cha redio nchini akiishutumu Simba kutaka kumpa hongo kwa ajili ya kufanikisha mpango wa kupanga matokeo.

Alidai Simba ilimshawishi afanye kosa kwenye mechi dhidi ya JKT Tanzania litakalomfanya aoneshwe kadi ya njano na kufikisha idadi ya kadi zitakazomsababisha akose mechi iliyofuata dhidi ya watani wa jadi katika soka ya Tanzania.

Hata hivyo, Kabwili aliyesimama langoni kwenye mechi dhidi ya Simba Februari 16, mwaka jana, Yanga ikifungwa 1-0, bao pekee la mshambuliaji Meddie Kagere dakika ya 72 alisema hakukubali kushiriki mpango huo.

Wakati mchezaji huyo akisubiri kwenda kwenye Kamati ya Maadili ya TFF, Klabu ya Simba imepinga na kukemea vikali kauli ya Kabwili.

Katika mtandao wao wa Instagram jana, Simba walisema wanapinga vikali kauli hiyo aliyoitoa juzi katika kituo cha Redio cha East Afrika, na kusisitiza kwamba inaamini kauli za aina hii kutoka kwa wachezaji ni za kuchukiza na sio za heshima ambazo zinaashiria upangaji wa matokeo ya mechi kama ilivyotuhumiwa na mchezaji huyo.

Ilisema: “Kauli hizi zina madhara makubwa kwenye uadilifu wa klabu ya Simba na uongozi wake, heshima kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania inawekwa mashakani kama kauli za namna hii hazitachukuliwa hatua stahiki”. Taarifa hiyo ilisema Simba inafurahishwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na TFF dhidi ya kauli kama hizi kwa vyombo husika.

“Simba inaamini jambo hili lipo mbele ya mikono ya vyombo husika na litachukuliwa hatua stahiki haraka,” sehemu ya taarifa hiyo ilisisitiza.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.