Inaelezwa uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti wa timu hiyo, Dk Mshindo Msolla, unatarajia kukutana na kiungo wake mshambuliaji, Mghana, Bernard Morrison kujadiliana ishu ya kumuongeza mkataba mpya kabla staa huyo hajashawishiwa kujiunga na wapinzani wao, Simba.
Timu hiyo inafikia maamuzi hayo ya kumuongezea mkataba baada ya kuridhishwa na kiwango cha mshambuliaji huyo katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara walipocheza na Singida United juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Namfua huko mkoani Singida. Morrison alisajiliwa na Yanga muda mfupi kabla ya usajili mdogo kufungwa Januari 15, mwaka huu.
Usajili wake ulifanikishwa na Kampuni ya GSM chini ya Mkurugenzi wa Uwekezaji wa kampuni hiyo, Injinia Hersi Said. Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, bosi wa GSM ambaye ni Hersi amepanga kukutana na mshambuliaji huyo kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya kuongeza mkataba huo mpya wa kuendelea kuichezea Yanga.
Mtoa taarifa huyo alisema bosi huyo amepanga kutoa kitita chochote cha fedha ili kuhakikisha mshambuliaji huyo haondoki na badala yake anaendelea kukipiga Yanga, ni baada ya kuvutiwa na kiwango cha mchezaji huyo.
Aliongeza kuwa kwa kushirikiana na kocha wa timu hiyo, Mbelgiji Luc Eymael watahakikisha wanamuongezea mkataba mwingine wa mwaka mmoja na miezi sita na kufanya ifikie miaka miwili kwani awali alisaini kandarasi ya miezi sita tu.
“GSM kamwe hawatakubali kuona mshambuliaji huyo akiondoka Yanga na kwenda kwenye klabu ya hapa nchini ikiwemo Simba, kama kuondoka basi iwe nje ya nchi.
“Na katika hilo tayari viongozi wa Yanga kwa kushirikiana na GSM ambao wanafanikisha usajili katika suala la pesa, wameweka mikakati ya kuhakikisha mshambuliaji huyo haondoki Jangwani.
“Wamefikia hatua hiyo baada ya kuona mkataba waliompa wa miezi sita ni mfupi ambao unamruhusu hivi sasa kufanya mazungumzo na klabu nyingine itakayomhitaji, hivyo baada ya kuridhishwa na kiwango hicho haraka wamepanga kumuongezea mkataba,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Morrison kuzungumzia hilo alisema: “Mimi sina tatizo na Yanga, nipo tayari kuongeza mkataba mwingine wa kuendelea kuichezea timu yangu hii mpya. Jumapili (kesho) nitakutana na uongozi kujadiliana kuhusu suala la kuongeza mkataba.
“Lakini kikubwa nitakachokiangalia ni maslahi pekee kwa maana ya kunipa kiasi cha pesa ambacho mimi ninakihitaji hivyo nitakuwa katika sehemu nzuri ya kusaini mkataba mwingine. “Labda niwaondoe hofu mashabiki wa Yanga kuwa, mimi sina mpango wa kuihama timu yangu hii mpya na hakuna mazungumzo yoyote niliyowahi kufanya tofauti na Yanga.
Post a Comment