KIUNGO mchezeshaji fundi Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ amewatoa hofu mashabiki wa Yanga na kuwasisitiza wazibeze kejeli za Simba.
Staa huyo mwenye mapenzi na Yanga, amesisitiza kwamba wanajua waliteleza wapi na kwamba muda si mrefu mashabiki wataanza kunogewa na kusahau tambo na mikogo ya watani zao.
Kiungo huyo mwenye uwezo wa kukaa na mipira, kuchezesha timu kwa kupiga pasi za mwisho za kufunga mabao alijiunga na Yanga kwenye usajili huu wa dirisha dogo akitokea AS Kigali ya Rwanda baada ya kuvunja mkataba.
Yanga tayari imecheza michezo mitatu mfululizo ya ligi kuu bila ya kupata ushindi, ikilazimishwa sare ya mabao 2-2 na Simba kabla ya kupoteza michezo dhidi ya Kagera Sugar na Azam FC. Jana jioni ilicheza na Singida United.
Niyonzima ambaye humpotezi kwenye mitaa ya Kinondoni na Sinza jijini Dar, alisema; “Ni kipindi ambacho lazima kila timu ikipitie ili kupata mafanikio ya timu yetu, kikubwa niwaombe mashabiki kuendelea kuwa watulivu wakati sisi wachezaji tukiendelea kuipambania timu yetu ili kupata matokeo mazuri.
“Tulikuwa katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, lakini tumeshushwa na tunapita kwenye wakati mgumu, kikubwa mashabii wetu wafahamu kuwa kila changamoto inakuwa na njia ya mafanikio, tutarejea tukiwa imara.
“Malengo yetu wachezaji ni kuchukua ubingwa wa ligi, hivyo ninaamini kwa kushirikiana na wachezaji, benchi la ufundi tutafanikiwa kama mnavyofahamu kocha wetu bado mpya hivi sasa yupo anaendelea kukiboresha kikosi chake kwa haraka ili kufi kia mafanikio,” alisema Niyonzima
Post a Comment