Baada ya hivi karibuni kuwepo kwa taarifa kuwa baadhi viongozi wa Simba kuwa na hofu na uwezo wa mshambuliaji Meddie Kagere katika kutupia, Wazungu kutoka Hispania wanamtaka straika huyu.
Kagere ambaye sasa anaongoza katika kuzifumania nyavu kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 11, amewahi kuhusishwa kutakiwa na klabu nyingi za Uarabuni lakini dili zote zilichomolewa na viongozi wake kwa kuwa timu ilikuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wakala wa Kagere, Patrick Gakumba alisema kuwa, klabu moja inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Hispania inamtaka Kagere haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kwenda kuiongezea nguvu katika harakati zake za kuhakikisha inapanda ligi kuu.
Gakumba aliongeza kuwa, klabu hiyo ambayo hakutaka kuitaja jina, ipo tayari kumnunua au kumchukua kwa mkopo. “Kagere amepata ofa kutoka katika timu moja inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ambayo kwa sasa siwezi kuitaja jina lake ila ni ya nchini Hispania.
“Timu hiyo ipo tayari kumnunua au kumchukua kwa mkopo na inachosubiri ni majibu yetu na imetutaka kuwapa majibu hayo haraka. “Kwa hiyo, hivi sasa nipo katika harakati za kuwasiliana na uongozi wa Simba juu ya hilo kwa sababu wenyewe ndiyo wana uamuzi wa kumuuza au kutomuuza kwani ana mkataba nao.
“Kama wataona dili hilo lipo vizuri basi unaweza kumuuza kwa sababu ni hela nzuri ambazo watapata kutoka kwa timu hiyo,” alisema Gakumba. Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ili azungumzie hilo, simu yake iliita bila kupokelewa
Post a Comment