BAADA ya kushuhudia ‘nyomi’ la mashabiki wa Simba, mshambuliaji mpya wa kikosi hicho, Deo Kanda, amekiri kuwa klabu hiyo ni noma, ikiifunika hata TP Mazembe ya DR Congo.

Kanda alipagawa na mashabiki wa Simba walioujaza Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, wakati wa mchezo wa kimataifa wa kirafiki wa Tamasha la Simba Day juzi dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.

Mchezo huo, pia ulikuwa maalum kwa kutambulisha wachezaji wapya, ambapo Simba walishinda mabao 3-1.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kanda alisema licha ya kucheza katika klabu kubwa Afrika, hawajawahi kuona mashabiki wengi kama alivyowaona wa Simba.

“Nimecheza TP Mazembe ni timu kubwa Afrika na nyingine, lakini sijawahi kuona siku uwanja umejaza mashabiki wengi kama hivi, ni kitu cha kwanza kukiona tangu nimeanza kucheza soka,” alisema Kanda.

Alisema kujitokeza kwa wingi wa mashabiki uwanjani, inawapa hamasa na kama wachezaji wanatakiwa kufanya kazi kwa ubora ili kuendelea kuwapa furaha wapenzi wao.

Kanda alisema wanakabiliwa na Ligi ya Mabingwa Afrika na michuano mingine, wanachotakiwa kufanya kama wachezaji ni kushirikiana kufikia malengo waliyojiwekea.

“Mechi hii ni mwanzo, tunakabiliwa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kama wachezaji tunatakiwa kufanya kazi yetu vizuri, kupata matokeo mazuri,” alisema Kanda.

Naye Francis Kahata, alionekana kupagawa na wingi wa mashabiki, akieleza kuwa hali hiyo ameiona Tanzania pekee inaonyesha watu wanavyopenda timu zao.

“Sijawahi kucheza mbele ya watu wengi kama hivi, ilinifanya niwe na hofu kidogo, ila nimefurahi sana nawashukuru mashabiki wa Simba wa sapoti hii,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kahata alisema mshambuliaji wa timu hiyo, Meddie Kagere ni mchezaji asiyechuja na si kitu cha ajabu kumuona anafunga ‘hat-trick’.

Kahata alisema anamfahamu vizuri Kagere ni mchezaji anayejituma na ushirikiano kwa wenzake, hali inayofanya kiwango chake kuendelea kukua.

Tags:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.