Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki saa 24 kabla ya dirisha la usajili Ulaya kufungwa, mshambuliaji wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta amevunja ukimya kuhusu hatima yake ya kucheza Ligi Kuu England.
Dirisha la usajili linafungwa leo saa sita usiku, lakini jina la nahodha huyo wa Taifa Stars, halimo katika orodha ya majina ya wachezaji wanaowindwa na klabu za Ligi Kuu England katika usajili wa majira ya kiangazi.
Samatta anayecheza klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji msimu uliopita alifunga jumla ya mabao 32 katika mashindano yote. Nyota huyo alifunga mabao 23 ya Ligi Kuu na tisa katika michuano ya Europa.
Akizungumza jana, Samatta alisema licha ya kubaki saa chache kabla ya dirisha la kufungwa, lolote linaweza kutokea katika usajili wake wa majira ya kiangazi.
Alisema ana mkataba wa miaka mitatu na KRC Genk na atakuwa tayari kuondoka endapo klabu inayomtaka itakubaliana na viongozi wa klabu yake kwa kuwa ndoto yake ni kucheza England.
Awali, Samatta alikuwa akitakiwa na klabu za England Aston Villa, Leicester City, Watford, Middlesbrough na Burnley zilizoonyesha nia ya kumsajili. Pia Galatasaray na Lille zilihusishwa na mpango wa kumsajili.
“Naheshimu mkataba wangu, sipendi kuzungumzia sana hilo kwa sababu linaweza kuondoa fikra na mawazo yangu kwenye ligi, msimu umeanza na nawajibika kuisaidia Genk kufanya vizuri, ndani ya muda sahihi kila kitu kitakuwa wazi,” alisema Samatta.
Mkurugenzi wa ufundi wa KRC Genk, Dimitri De Conde alisema bado wanamhitaji Samatta, lakini watakuwa tayari kumwachia endapo tu itapatikana klabu sahihi watakayofikia mwafaka kuhusu maslahi.
Conde alisema mshambuliaji huyo ni miongoni mwa nyota watatu waliopo sokoni akiungana na wengine Joakim Maehle na Sander Berge.
“Tuna hofu ya kumpoteza, tunamhitaji Samatta katika mashindano makubwa, kama bodi tunahitaji kuwekeza ili tuwe na nguvu kubwa ya ushindani.
“Tunajua ndoto ya Samatta ni kucheza England tusubiri tuone nini kitatokea kwa sababu si dhamira yetu kukwamisha anachopenda na ukizingatia alitoa mchango mkubwa kwetu,” alisema Conde.
Baba wa Samatta, Ally Pazi alisema alimshauri mwanaye kujiunga na Aston Villa kwa kuwa moja kwa moja atapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.
“Nasikia hiyo timu ya England (Aston Villa) imepanda daraja, binafsi naona itakuwa rahisi kupata nafasi kikosi cha kwanza. Akizoea ligi ni rahisi kuhamia klabu nyingine,” alisema Pazzy.
Aston Villa na Leicester City ziliweka mezani Pauni 12 milioni zilizokataliwa na KRC Genk ambayo ilitaka Pauni 15 millioni.
Mchezaji huyo alijiunga na KRC Genk Januari 29, 2016 akitokea TP Mazembe ya DR Congo ambayo aliiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, aliondoka Afrika akiwa na tuzo ya uchezaji bora kwa wachezaji wa ndani.
Post a Comment