KOCHA Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema kambi waliyoweka Afrika Kusini ilikuwa nzuri kutokana na huduma bora kuanzia chakula na malazi.

Aussems aliyasema hayo juzi baada ya kurejea na kikosi chake kwa ajili ya maandalizi ya wiki ya Simba inayatorajiwa kuhitimishwa wiki ijayo.

Akizungumza baada ya kurejea juzi, kocha huyo alisema: “tunashukuru Mungu tumerejea salama, tulikuwa na wiki tatu nzuri Afrika Kusini katika kambi tulioishi vizuri, tumekula vizuri na kila kitu kilikuwa kiko vizuri.”

Kocha huyo alisema changamoto iliyopo ni ratiba ya timu ya taifa kushindwa kuwapa nafasi wachezaji wake saba kukaa pamoja kwa muda mrefu kwenye mazoezi baada ya kuitwa kuitumikia katika mchezo dhidi ya Kenya.

“Changamoto iliyopo wachezaji saba wanacheza katika timu ya taifa bado tulikuwa hatujakaa pamoja kwa muda mrefu kwa ajili ya kutengeneza kikosi,”alisema.

Wachezaji saba wanaotumikia timu ya taifa ni Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, John Bocco na Hassan Dilunga.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara wakiwa Afrika Kusini walicheza michezo kadhaa ya kirafiki na kutopoteza hata mmoja ikiwa ni sehemu ya kujiimarisha kwa msimu ujao wa ligi na michuano ya kimataifa.

Walicheza dhidi ya Orlando Pirates na kutoka sare ya bao 1-1 matokeo sawa waliyopata katika mchezo mwingine dhidi ya Township Rollers, wakashinda 4-1 dhidi ya Platnum Stars na 4-0 dhidi ya Orbet Tvet.

Simba kwa sasa ipo kwenye wiki ya Simba kuelekea tamasha la Simba day litakalofanyika Agosti 6.

Leo watachangia damu Mbagala na Ubungo kabla ya kutembelea ofisi za wadhamini wao mbalimbali. Mabingwa hao wa Bara wanatarajia kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki kwenye kilele cha wiki yao Agosti 6 mwaka huu dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, wakitarajiwa kutambulisha kikosi chao cha msimu kabla ya kupaa ndege kuelekea Msumbiji kuwafuata Ud Do Songo.

Katika hatua nyingine, Simba jana iliingia mkataba na benki ya Equity itakayotengeneza kadi kwa wanachama ambazo hazitakuwa tofauti na kadi nyingine za benki.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu wa Simba Crescentius Magori alisema kadi hizo zitawasaidia kujua wanachama wao halali pamoja na mashabiki wao.

“Kutakuwa na kadi za aina mbili, moja Simba bank ambayo ni kwa ajili ya wanachama na nyingine ni fans card ambayo itamhusu shabiki wa Simba na zitaanza kutolewa Septemba mosi,”.

Alisema kadi hizo zitatumika kwenye kununua tiketi na kuichangia timu ambapo kwa mwezi kila mwenye kadi atachangia sh 1000 kwenye klabu yake.

“Kadi ni sh 10,000 na sh 2500 zinakwenda kwa klabu inayobaki ni mwanachama kwenye akaunti yake… nawaomba mashabiki na wanachama wa Simba wafungue akaunti kwenye benki ya Equity ili kupata kadi hizo,” alisema.

Tags:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.