Na Saleh Ally
MSIMU mpya unakaribia kuanza na hali inaonyesha ushindani utakuwa wa juu na hasa kama wanaosimamia mpira wa Tanzania watakuwa makini.


Kutakuwa na ugumu kwa kuwa timu nyingi zinaonekana kubadili mfumo wa maandalizi yao ya mwanzo ya msimu. Ukitulia utagundua safari hii kila upande umefanya mambo kwa umakini mkubwa.


Ukiangalia mfano mzuri Azam FC, wamepaki nyumbani baada ya kuwa wametokea Rwanda kwenye michuano ya Kombe la Kagame na kufika fainali. Pamoja na hivyo, wamerejea nyumbani na kufanya mazoezi mazuri na makali kujiandaa na msimu mpya.



Tumeona KMC nao wanafanya kazi nzuri na wanajipanga hasa kutokana na kuwa na maandalizi yenye mpangilio. Ninaamini kuna timu huenda zikawa hazionekani sana lakini zinaendelea na maandalizi.


Kuripotiwa sana kwa Simba na Yanga, au Azam na KMC kwa kuwa ndio zinaiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa, inawezekana zimechangia hata timu nyingine nazo kuongeza umakini katika maandalizi ya awali kabla ya kuanza kwa msimu.


Wakati haya yakiendelea, kuna mengi yanatokea ya kujifunza. Kila mtu anaweza kuchagua anataka kujifunza wapi lakini ninaona wachezaji wawili, ninaweza kuwatumia kama mfano katika hili.


Mkongomani, Papy Kabamba Tshishimbi ni kati ya viungo bora anapocheza uwanjani. Wakati akitua nchini na kujiunga na Yanga kutoka Mbabane Swallows, sote tunakumbuka namna alivyokuwa katika kiwango bora kabisa.


Baada ya muda, Tshishimbi aliyumba hadi kufikia kuwa mchezaji wa benchi. Kitu kizuri zaidi, hakukuwa na kisingizio kwa kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ni raia wa DR Congo kama ilivyo kwa Tshishimbi. Jibu lilikuwa ni kiungo huyo amezembea.



Hali yake imewatokea wachezaji wengi sana wa kigeni, waliozinduka waliendelea na kung’ara zaidi lakini wengi walipotea kabisa. Hii inatokana na “ukarimu” wa Watanzania uliopitiliza.


Kwa Afrika hii, huenda nchi yetu inaweza kuongoza kwa ukaribu na isipokuwa hivyo, basi angalau nafasi ya tatu. Watu wako tayari kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wageni wanajisikia wako nyumbani.


Katika hali ya kawaida, ilionekana Tshishimbi anaweza hata kuachwa na Yanga. Kengele hii ilimfanya aamke na kurejea kazini kwa nguvu na utaona alivyoumaliza msimu akiwa katika kiwango bora kabisa.


Sasa Tshishimbi ameuanza msimu katika kiwango bora kabisa ikiwezekana hata kuliko alivyoumaliza. Kama umeona mechi za kirafiki za Yanga au mazoezi yao, basi Tshishimbi amekuwa mfano wa kuigwa.


Hii inaonyesha aliumizwa na kile alichokosea, lakini amejua kuwa Yanga inakwenda kucheza michuano ya kimataifa na kuna nafasi ya yeye kujipatia maisha zaidi ya alipo sasa.


Mfano kama watafanikiwa kuvuka dhidi ya Township Rollers ya Botswana, ataendelea kujitangaza. Ikishindikana, mechi mbili dhidi ya Waswana hao zitakuwa msaada kwake kujipatia soko iwe kwa wapinzani hao, watakaoshuhudia wengine au hata Yanga wenyewe wakati utakapofikia muda wa kuongeza mkataba.


Achana na Tshishimbi, kambi ya Simba ilikuwa nchini Afrika Kusini. Ninaamini kila mchezaji alijituma, lakini angalia Meddie Kagere. Mfungaji bora na mchezaji tishio zaidi wa Simba kwa msimu wa 2018/19.


Kagere alikuwa anajituma utafikiri ni mchezaji aliye benchi na angetamani kupata namba ya kucheza katika kikosi cha Simba.


Licha ya kuwa mfungaji bora msimu uliopita, hii haikumfanya yeye ajisahau na kuanza kuwa msumbufu, kuchelewa kambini au mazoezini. Kutaka anyenyekewe au kutaka kusikilizwa yeye tu na kadhalika.


Badala yake, amekuwa sehemu ya wachezaji mfano hasa wa kuigwa na anaonyesha ana njaa. Anataka kufanya vizuri zaidi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa faida ya Simba na yeye mwenyewe.


Huu ni mfano mdogo tu wa watu wanaojitambua na wanajua wanafanya nini. Hawalaumu au kulalamikiana, hawana mawazo ya kupiga majungu na hakuna kelele nyingi.


Ni hivi; aliyefanya vizuri amejituma zaidi na kutaka kufanya vizuri zaidi ya alivyofanya. Ambaye aliharibu kajirekebisha na sasa anapambana kufanya vizuri zaidi na zaidi. Hawa ni wenye ndoto wanaotaka kuzidisha kuzifikia ndoto zao. Hivyo wawe mfano na Wachezaji wazalendo ambao ni ndugu zetu, wajue wanapaswa kuangalia mifano hii.



Unapoharibu unakuwa na nafasi ya kujirekebisha na baadaye kufanya bora zaidi lakini si kwa maneno mengi na kelele tu. Lakini ukifanya vizuri msimu mmoja, isiwe sababu ya kuanguka msimu mwingine, badala yake iwe chachu ya kufanya vizuri zaidi.
Tags:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.