NOMA KWELI, LUKAKU AMWAGA MBOGA KUHUSU MAN UNITED
MILAN, Italia
HATIMAYE straika wa Inter Milan, Romelu Lukaku amefunguka na kuitupia lawama klabu yake ya zamani, Manchester United kwa kushindwa kumlinda mchezaji huyo raia wa Ubelgiji.
Hivi karibuni, straika huyo mwenye umri wa miaka 26 alijiunga na Inter Milan kwa dau la pauni milioni 75, baada ya kuwatumikia mabingwa wa zamani wa England kwa misimu miwili.
Msimu uliopita, Lukaku alifunga mabao 12 katika Ligi Kuu England, lakini hakuwa chaguo la kwanza kuelekea mwishoni mwa msimu, baada ya kocha wa timu hiyo, Ole Gunnar Solskjaer kumpa kipaumbele Marcus Rashford kuongoza mashambulizi.
Licha ya kupata wakati mgumu wa kufunga mabao, Lukaku anaamini kuwa malalamiko juu yake hayakuwa sahihi, pia, alidai Manchester United walishindwa kuwalinda akina Paul Pogba na Alexis Sanchez pindi timu inapofanya vibaya.
“Mashabiki wanatafuta wa kumpa lawama pindi timu inapofanya vibaya, atakuwa Pogba, mimi au Sanchez, ni sisi watatu ambao tulitajwa mara nyingi, kwa upande wangu, nililichukulia kwa njia nyingi.
“Timu ilishindwa kutulinda, hakuna aliyekemea kilichokuwa kinatokea, wakati wote tulikuwa wakulalamikiwa tu.
“Hata alipoingia Solskjaer, watu wengi walifikiri siwezi kuwa sehemu ya kikosi chake, hayo ni mawazo yao lakini nilijisikia vibaya sana,” alisema.
Hata hivyo, wengi walikuwa wakishangaa kwanini straika huyo alikuwa akifanya vibaya ndani ya klabu yake lakini alikuwa moto wa kuotea mbali akiwa na timu ya Taifa ya Ubelgiji.
Hilo pia alilitolea ufafanuzi Lukaku ambaye anaamini ushirikiano anaopewa na wenzake kwenye kikosi cha Ubelgiji ulimfanya ajihisi yupo sehemu ya timu.
“Kwa upande wangu, ilikuwa ikinishangaza jinsi mambo yalivyokuwa yakienda, nilionekana kuwa mchezaji mbaya nilipokuwa na klabu, lakini nilipokuwa Ubelgiji nilikuwa tofauti.
“Kipindi chote nilichokuwa na timu ya taifa, nilijihisi kuwa sehemu ya timu, nilipewa ushirikiano na wenzangu kwa wakati wote, mazoezi, kwenye mechi hata kambini,” alifafanua.
“Kuna kitu hakipo sawa, ni mimi? Sikucheza wiki tatu za mwisho wa msimu na nilikuwa na wiki tatu zingine kabla ya kwenda kuitumikia Ubelgiji, lakini hakukuwa na mtu aliyelaumu hilo,” aliongeza.
Manchester United haikufanya vizuri msimu uliopita, wamekosa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kumaliza nafasi ya sita, walimtimua Jose Mourinho na kumpa kazi Solskjaer katikati ya msimu.
Straika huyo wa zamani wa Everton, alidai kuwa tangu ajiunge na Manchester United hajawahi kucheza kwa kiwango cha juu kama ilivyokuwa ndani ya Goodison Park.
Pia, alijaribu kukichambua kikosi cha msimu huu na kuamini kinaweza kufanya mambo makubwa lakini kama watajituma zaidi.
“Nilinyoosha mikono juu, nafikiri sikucheza kwa kiwango change tangu nilipojiunga na Manchester United, lakini sikuwa mchezaji pekee niliyecheza vibaya kama watu wanavyosema.
“Najua mchezo wa soka una mambo mengi, mpaka sasa nimepitia changamoto nyingi, nipo hapa kucheza mpira, naamini nitafanya vizuri.
“Manchester United wana timu nzuri, vipaji vingi vipo lakini haviwezi kuwasaidia kama watashindwa kujitoa kwa ajili ya timu, huu ni wakati wa kujenga timu mpya, watafanikiwa,” alidai Lukaku.