JOTO la mchezo wa watani wa jadi katika ngwe hii ya lala salama unaotarajiwa kupigwa Machi 8, limewahi sana tofauti na mchezo wa raundi ya kwanza, si jambo la kushangaza sana kuona hali hii kutokana na ukweli kuwa kila timu sasa hivi inajitahidi kuweka hesabu zake vizuri tayari kwa ajili ya kufunga msimu.
Simba inaingia katika mchezo huu ikiwa na mawazo ya kusaka ushindi kwa hali yoyote ili kujiweka vizuri katika mbio za kutetea ubingwa wake kwa mara nyingine tena, Yanga wao wanaingia katika mchezo huu wakiwa na nia ya kutaka kufufua matumaini yao ya kushindania ubingwa msimu huu.
Mchezo huu unatarajiwa kuwa na ushindani zaidi ya ule wa raundi ya kwanza hasa kwa sababu zipo sura mpya na za hatari kutoka pande zote mbili zinazotarajiwa kukichafua katika mchezo huu, Simba itaingia katika mchezo huu ikiwa na hasira za kupokonywa tonge mdomoni katika mchezo wa Januari 4, Yanga nao wataingia katika mchezo huu wakijiamini zaidi baada ya kufanikiwa kupindua meza kibabe katika mchezo wa kwanza.
Mara nyingi mchezo huu hutawaliwa na matukio mengi ya utovu wa nidhamu ambayo pia ni ngumu kwa waamuzi kuyaona kutokana na presha inayokuwepo kwa wachezaji kwa timu zote, hivyo ombi langu kwa TFF ni kuhakikisha wanachagua waamuzi bora na kusimamia maandalizi yao ili kuwaongezea ufanisi na kupunguza matukio ya utovu wa nidhamu kama yaliyotokea katika mchezo uliopita.
Ukiachana na suala la waamuzi, ombi jingine kwa TFF ni kuhakikisha maandalizi ya mchezo huu yanakuwa ya wazi na kuaminika, pia ni muhimu kusimamia kanuni na sheria ipasavyo ili kuondokana na minong’ono ya madai ya vyumba kupuliziwa madawa au timu kuingia uwanjani kwa kutumia milango isiyo rasmi, mambo ambayo hupunguza sifa ya mpira wetu na kutudharaurisha.
Huku kwetu mitaani tambo za mashabiki zimeshaanza kila mmoja akilinadi chama lake kuwa litaibuka na ushindi katika mchezo huu na wengine hata kudiriki kutabiri magoli ya kufunga na kufungwa katika mchezo huu kitu ambacho ni kawaida katika ushabiki ila muhimu lisizidi kwani kama litazidi linaweza likasababisha mashabiki kuaminishana mambo ambayo si uhalisia ikawa shida uwanjani.
Hivyo ni muhimu sisi mashabiki tukaendelea kujikumbusha kuwa siku zote mechi za watani wa jadi hazijawahi kuwa rahisi na wala hazitabiriki, kwa kujua uhalisia huo hatupaswi kwenda na matokeo yetu uwanjani bali tusubiri uamuzi wa zile dakika tisini kujua nini tumevuna katika timu zetu.
Mwisho kabisa ni imani yetu kuwa TFF itapanga viingilio rafiki ili mashabiki wengi waweze kushuhudia burudani ya mchezo huu unaovuta hisia za mashabiki wengi katika ukanda huu wa Afrika mashariki na kati na kwingineko duniani
Post a Comment