PAPY Tshishimbi, nahodha wa Yanga amesema kuwa kwa sasa ana ofa nyingi mkononi ambazo amezipata kutoka kwa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ikiwa ni pamoja na Simba huku nyingine zikitoka nje ya nchi.
Nahodha huyo raia wa Congo amekuwa kwenye ubora wake tangu alipotua Jangwani msimu wa 2018 akitokea Klabu ya Mbabane Swallows ambapo kwa msimu huu amecheza mechi 23 za Ligi Kuu Bara za Yanga kati ya 27 na ametoa pasi moja ya bao lililofungwa na Tariq Seif mbele ya Biashara United.
Kwa sasa mkataba wake wa mwaka mmoja amesema umebakiza miezi minne ambapo kanuni za Shirikisho la Soka Duniani, Fifa unampa ruhusa ya kufanya mazungumzo na Klabu yoyote inayomhitaji.
Tshishimbi amesema kuwa amefanya mazungumzo na klabu yake ya Yanga na bado hawajafikia makubalino endapo watashindwa kuelewana anaweza kuondoka na kuendelea na maisha mengine.
“Niliongea na Eng.Hersi Said aliniambia kwamba anataka kunipa mkataba wa miaka miwili nilikubali lakini sikusaini hivyo kwa sasa ninasubiri kuona nini kitatokea kwani timu nyingi zimekuja kwangu na nimeskiliza ofa zao kwani ukiwa mchezaji huwezi kukataa ofa.
“Sio Simba pekee ambao wamenifuata ni timu nyingi,furaha ya mchezaji ni kuona anafuatwa na timu nyingi na siwezi kukataa nini ambacho wananiambia ila kitu kikubwa ambacho ninaangalia ni kuskiliza maslahi kwanza, iwe Simba ama timu nyingine mimi nitasaini kwani mimi ni mchezaji.
“Kama Yanga wananihitaji nipo na Yanga kama Yanga watasema hawanihitaji basi nitatafuta sehemu ya kwenda na maisha yataendelea ninapenda kucheza ndani ya yanga lakini ni lazima ofa yangu nami niifurahie, mimi ninasema kweli lolote linaweza kutokea kwani nilisaini mkataba wa mwaka mmoja na sasa imebaki miezi minne,” amesema Tshishimbi.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, kupitia Ukurasa wake wa Instagram aliandika kwamba miongoni mwa wachezaji kwenye nafasi ya viungo anaopenda kuwaona wakicheza ndani ya Simba ni pamoja na Tshishimbi.
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa iwapo Tshishimbi atasajiliwa ndani ya Simba kutaongeza mfumo wa uchezaji kwenye kikosi hicho ambapo itatengenezwa pacha yake na Jonas Mkude ambaye amekuwa mhimili ndani ya Simba kwa upande wa ukabaji.
“Tshishimbi ni mchezaji mzuri na anauwezo mkubwa wa kupata namba kikosi cha kwanza, pacha yake inaweza kufiti akianza na Mkude, pia hata kwa mtindo ambao anacheza Deo Kanda, Clataus Chama, italeta matokeo chanya na upana wa Kocha Mkuu kuchagua mfumo,” ilieleza taarifa hiyo.
Post a Comment