UONGOZI wa timu ya Orlando Pirates umeweka wazi kuwa upo tayari kumuachia straika wao, Mzambia, Justin Shonga katika usajili ujao iwapo watafikia muafaka na timu inayomuhitaji.
Kauli hiyo imetolewa ikiwa ni siku chache tangu kuwepo kwa taarifa za Mzambia huyo kuhitajika na Simba kwa ajili ya msimu ujao ambapo timu hiyo inatarajiwa kushiriki michuano ya kimataifa.
Mzambia huyo alijiunga na Orlando mwaka 2017 ambapo katika msimu wake wa kwanza alifanikiwa kucheza mechi 19 akifunga mabao manne. Msimu uliopita alifunga mabao sita katika mechi 29.
Taarifa kutoka kwa vyanzo vya uhakika Afrika Kusini vinadai kuwa, Simba wana nafasi kubwa ya kumpata mshambuliaji huyo iwapo wataweka pesa ya kutosha kutokana kocha wa sasa wa timu hiyo kutomkubali.
Spoti Xtra limezungumza na Ofisa Habari wa Orlando, Thandi Merafe kwa njia ya simu moja kwa moja kutoka Afrika Kusini, ambaye alisema: “Kwanza suala la Simba kumuhitaji Shonga bado halijafika kwenye meza yangu, kwa sasa ligi yetu imesimamishwa kwa muda kutokana mlipuko wa hili janga la Corona.
“Suala la yeye kuongeza mkataba ni kweli tumemuongeza na hakuna timu ambayo inakataa kuuza mchezaji iwapo maslahi yanapokuwa mazuri, ila kwa sasa ni jambo la kusubiri huu wakati upite ili kuweka wazi kila kitu.”
Post a Comment