WAKATI mwingine unajaribu kutafuta majibu ya tatizo lilipo unaishiwa nguvu na kushindwa kujua nini ufanye kutokana na aina ya tatizo ambalo lipo mbele hii inatokana na yale yanayokuzunguka kufurahisha na kuhuzunisha.
Kwa sasa tupo kipindi kigumu cha mpito ambapo hakuna burudani ya soka inayoendelea ulimwenguni hili ni muhimu kulizingatia na wakati wa kutafuta majibu ni muhimu kufikiria namna ya kuendelea kuchukua tahadhari.
Nimeanza hivyo kutokana na namna ambavyo watu wanaamua kujipa hofu kubwa kwa kupambana na tatizo la Virusi vya Corona ambapo kila mmoja anataka kuonyesha kwamba naye anaweza kuwa msemaji wa suala hili.
Kiukweli suala hili sio la kuchukulia mzaha na kufanya kila kitu unakuwa mjuaji sio busara kujua ni jambo la msingi na kuhitaji kujua pia ni muhimu hivyo ushauri wangu kwa sasa watanzania na wapenda burudani ni muhimu kupunguza ujuaji.
Kanuni za afya zifuatwe bila kupuuziwa na tahadhari kila siku ni muhimu isifanywe kwa mazoea leo unafanya kesho unaachana nayo iwe ya mwendelezo kwani ingekuwa tunaendelea na desturi zetu za zamani leo ingekuwa ni kesi ndogo kumkumbusha mtu kunawa mikono.
Pia kingine ni kwa upande wa familia ya michezo ninaona kumekuwa na utani mwingi hasa kwa hili linaloitwa program za kufanya ili wachezaji wawe bora na kulinda vipaji vyao.
Iwapo hali itakuwa shwari, ligi inatarajiwa kurejea hivi karibuni na ile shughuli ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa shauku itaendelea na zile burudani za marefa na wachezaji zitarudi.
Kumekuwa na mkanganyiko mkubwa ambapo wachezaji wanakuwa na mpango wao huku makocha pia wakiwa na mtazamo wao kuhusu namna ya kutimiza program hizo.
Wachezaji wengine watakuambia hawajapewa program na wengine ukiwauliza watakuambia wamepewa program sasa hapo ni tatizo lipo ndani ya timu ama kwa wachezaji lisipotafutiwa dawa litakuja kuleta matokeo ya ajabu hapo baadaye.
Ukweliupo wazi ikiwa kuna baadhi ya wachezaji ndani ya timu moja wamepewa program na wengine hawajapewa huku kwa upande mwingine kuna timu ambazo hazina kabisa program za mazoezi unadhani nini kitatokea?
Ligi itakaporejea kazi itakuwa kwa wachezaji kuanza kujijenga upya huku makocha wakiwa na kazi ya kutengeneza kikosi upya jambo ambalo litachukua muda wakati mechi zimebaki chache.
Ukitazama msimamo utagundua kwamba timu inayoshika nafasi ya mwisho Singida United imebakiwa na mechi tisa baada ya kucheza 29 huku Simba imebakiwa na mechi 10 baada ya kucheza 28 ndipo utajua kwamba iwapo ligi itarejea hakutakuwa na muda wa kujipanga.
Kitu cha muhimu kwa sasa ni makocha kuhakikisha kwamba wanatoa program kwa wachezaji wote huku wale ambao hawajapewa program waelezwe cha kufanya ili kuwa bora na kulinda uwezo wao.
Kila mchezaji asisahau kwamba jukumu lake ni kucheza na kipaji chake na lazima akilinde kwani hiyo ni kazi yake huku timu ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja zitumie muda huu kurejea kwenye ubora wao.
Iwapo hali ya mazoea itaendelea kwa timu kutokuwa na mpango kazi zitakaporejea zitakutana na mlima mwingine wa kufanya ilihali mechi zipo chache, tahadhari muhimu na mazoezi pia ni muhimu.
Post a Comment