NA SALEH ALLY
JUZI niliitwa na Mkurugenzi na Mwenyekiti wa makampuni yaliyo chini ya Global Group, huyu ni Eric Shigongo ambaye alinieleza wazo lake kuhusiana na anachoona tufanye kuhusiana na kupambana na ugonjwa wa Corona.
Kila mmoja wetu anajua namna Corona inavyoisumbua dunia kwa sasa na tayari Tanzania tuna wagonjwa 13 ambao wameambukizwa ingawa tunashukuru kuwa baadhi wameanza kupona kabisa ambalo ni jambo jema kwetu.
Shigongo alinieleza wazo lake namna tunavyoweza kupambana na ugonjwa huu tukiungana na jamii ya wasomaji, wasikilizaji na watazamaji wa vyombo vyetu.
Kwa sasa, sisi Global Group ndiyo Jumba la Vyombo vya Habari kubwa zaidi kuliko nyingine zote hapa Tanzania, kwa kuwa tuna magazeti makubwa zaidi ya michezo kwa maana ya Championi na Spoti Xtra, magazeti Pendwa yasiyo na mpinzani lakini upande wa electronic tuna redio inayoongoza Online (+255 Global Radio) na runinga inayoongoza Online kwa maana ya Global TV Online.
Kuanzisha kampeni kwa vitendo kuungana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa wakati huu ni jambo sahihi kabisa.
Hauwezi kuwa unashirikiana na watu wako, rafiki zako au majirani zako wakati wakiwa na furaha tu. Kipindi hiki wako wenye hofu na inasababisha kupotea kwa utamaduni wa maisha ya kawaida ya Kitanzania ambayo huambatana na utulivu bila ya hofu hata punde.
Mara moja nililichukua wazo hilo la Mwenyekiti Shigongo kama mtendaji na kuanza kulifanyia kazi nikishirikiana naye pamoja na vijana wengine wa hapa ofisini kwetu na kazi ya kutengeneza ndoo, ununuzi wa dawa na kadhalika ikafanyika.
Wakatafutwa watu maalum wakiwemo wataalamu kwa ajili ya kazi hiyo. Ukiangalia kwa haraka unaweza kuona ni kazi ndogo lakini la, ilihitaji utulivu, uharaka lakini umakini katika utekelezaji.
Sasa tayari tuko katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam tukiendelea kunawisha watu kuhakikisha wanakuwa salama na kupambana kuitokomeza Corona.
Hili si jambo la kubeza hata kidogo, najua wakati mwingine kwenye vyombo vya habari wakiona watu wameanzisha jambo wao wasingependa kushiriki. Wanaweza kuona aibu kuwa wanaonekana wanaiga.
Binafsi najua tumeanzisha vitu vingi sana kwenye magazeti, redio na TV na wengine wakafuatia. Kwa mwendo huu itakuwa vizuri na hili vyombo vingine vya habari walifuate ili tuungane na Serikali yetu pamoja na jamii yetu kupambana na Corona kwa juhudi kuu kabla haijawa tishio kuu hapa kwetu.
Tufanye hivi kwa nguvu kubwa, tuionyeshe jamii kuwa tunaweza kuwa nao karibu. Hakuna haja ya kuona au kujisikia vibaya kwa kuwa Global Group wameanzisha basi tutaonekana tumeiga.
Kuiga vitu vizuri kama vile ambavyo wenzetu mmekuwa mkichukua kwetu si jambo baya, ndio maendeleo na mzunguko wa uzalishaji au uanzilishi wa vitu vipya.
Shida ya Corona hauwezi kujua itampata nani na wakati gani, huwezi kujua unaweza kuingiaje katika tatizo kwa kuwa mihangaiko ya maisha haikupi nafasi ya utulivu wa asilimia mia. Hivyo kama “StayHome” haijaingia kwetu na kuwa tatizo, tuanze sasa kupambana na huyu adui Corona, iwe kwa kuandika, kutangaza lakini kwa vitendo kama Global Group.
Hivyo huu ndio wakati mwafaka kama wanahabari, tuungane kupambana na Corona kwa ajili ya jamii yetu. Tuipe nguvu Serikali katika hili na tujisaidie wenyewe kwa kuwa ugonjwa huu hauchagui iwe tajiri au masikini, maarufu au asiyejulikana na mifano mingi tunayo.
Post a Comment