Na Saleh Ally
NIMESKIA tafrani iliyotokea Yanga hadi kusababisha baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga kujiuzulu.

Nilielezwa kuwa kuna baadhi ya wajumbe walihoji baadhi ya mambo wakiona kama wadhamini wao GSM wanavuka sana kufanya mambo yasiyowahusu na Uongozi au Kamati ya Utendaji kutohusishwa.

GSM wakakerwa na hilo na kuamua kuandika barua wakitaja wanayofanya kusaidia klabu na kuamua kukaa kando wakiahidi watafanya yale ya kimkataba tu.

Hapo ndipo tafrani lilipoanza na usuluhishi ukachukua nafasi kubwa. Kumbuka hapa kuna anayetoa fedha yake na mwenye klabu yake ambaye si mbunifu, licha ya utegemezi anataka awe na nguvu ya kila kitu.

Baada ya muda mambo yamekaa sawa na wasiokubaliana na hilo, wameamua kujiuzulu.

Hili halina tofauti kubwa na lile la Simba siku MO DEWJI alipoamua kujiuzulu. Nilipohoji likanisababishia matatizo, chuki isiyoisha hadi leo, jambo ambalo halijawahi kunipa hofu kwa kuwa naamini ninachosema ni ukweli tena bila ya woga.

Leo sina haja na MO DEWJI wala GSM, badala yake ni wanachama na viongozi wa Yanga ambao mmekuwa mnaishi maisha ya ushindi wa msimu mmoja baada ya hapo mnaanza maisha mapya ya msimu mwingine.

Hamna mipango ya muda mrefu ndio maana 1990 ndio 2000 na ndio 2020. Maendeleo kiduchu na mabadiliko ya jezi yanawafanya muone mmepiga sana hatua lakini uhalisia nyie ni TEGEMEZI SUGU wa kutupwa.

Hawa wafanyabiashara wanaingia wakiwa na mambo mawili na kubwa moja la MFANYABIASHARA linachukua 90% na mapenzi ni 10% au chini ya hapo.

Hivyo lazima wafaidike au kukuza Biashara zao kutokana na wanachotoa na tofauti yao na nyie wao wanataka kwenda mbele, wanawaza Biashara ambayo kuifanya kitu cha kwanza lazima uanze KUKUA jambo ambalo hamjawahi kuliwaza zaidi ya furaha ya KUMFUNGA MTANI ili kesho muwatanie kwa kuwaita VYURA au MIKIA.

Simba na Yanga zina thamani kubwa hadi wafanyabiashara kama MO Dewji au GSM wanazikimbilia, wanajua kuna fursa na faida iliyopo ndani yake.

Ajabu walizonazo hawaoni kwa kuwa macho yao hayaoni na miwani yao ni DUNI na ndio maana wanapokaa pamoja, WANAOONA na WASIOONA, milele imekuwa HAPAKALIKI.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.