Na Saleh Ally
KATIKA Gazeti la Spoti Xtra jana Alhamisi, kiungo nyota wa Yanga, Bernard Morrison, alizungumzia mambo mbalimbali likiwemo suala la namna ambavyo amevutiwa na mashabiki wa soka nchini.


Morrison, raia wa Ghana, alisema kuwa mashabiki wa soka nchini na hasa wa Yanga, wamekuwa na ushawishi wa aina yake hajawahi kuona.


Maana yake hata wale mashabiki wa klabu kongwe Afrika na maarufu nchini Afrika Kusini ya Orlando Pirates, hawawafikii mashabiki wa Yanga kutokana na ubora wa ushangiliaji.


Mahojiano haya yaliyofanyika nyumbani kwake Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, yanaendelea.


Morrison ndiye aliyefunga bao pekee wakati Simba ikilala kwa bao moja dhidi ya Yanga katika mechi ambayo ilionekana kwa mara nyingine Simba wakiwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi lakini mwisho wa mchezo, wao ndio wakalala kwa bao hilo moja lilifungwa kwa mkwaju wa adhabu na Morrison. Faulo hiyo ilipatikana baada ya yeye kuangushwa na kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude.


Ilikuwaje ukapiga ile adhabu dhidi ya Simba?
“Unajua sikutakiwa kupiga ule mpira kwa kuwa si majukumu yangu, binafsi si mtaalamu wa mipira iliyokufa, lakini niliona kuna nafasi ya kufanya hivyo.


“Kwa kuwa nilikuwa nimefanyiwa faulo, wakati nainuka Juma (Abdul) alisogea pale kwa ajili ya kutaka kuupiga mpira. Kwa maelekezo ya kocha alitakiwa apige faulo kama krosi na kina Lamine, Tshishimbi na wengine warefu wangekwenda kwa ajili ya kupiga kichwa.


“Mimi niliona kama kuna nafasi ya kufunga, nilichokifanya nilijaribu kuchungulia na kumuomba Juma kuwa aniachie ule mpira ninaweza kupiga moja kwa moja na kufunga.


 “Kitu kizuri naye alikubali vizuri kabisa, bila yeye isingekuwa vile. Nami nikafanya vile na kufunga. Wakati narudi nyuma nilijua nitafunga kwa kuwa niliangalia namna kipa alivyokaa na ukuta. Nikaona mambo mawili yakifanyika basi nitafunga. Kwanza ni spidi ya mpira lakini kulenga sehemu sahihi.


 “Hata wakati nakwenda kuupiga ule mpira nilikuwa na matumaini makubwa nitafunga. Hivyo utaona hata kabla ya kupiga niliona hivyo, hii inatokea mara kadhaa kwa wachezaji wengi watakuwa wananielewa.


“Nilisikia raha sana, kwa kuwa wakati tukiingia uwanjani nilitamani sana kufanya lolote kuisaidia timu kushinda. Mfano kutoa pasi ya bao, kucheza vizuri zaidi na suala la kufunga sikuwa nimelipa nafasi kubwa kwa kuwa huwa naingia uwanjani kwa lengo la kusaidia timu ishinde. Bahati nzuri ikatokea nimefunga bao, lilikuwa ni jambo zuri zaidi.”


Baada ya kufunga labda nini kilitokea kwako ambacho huenda haukukitegemea kabisa?
“Niwe mkweli hapo, hakika nilishangazwa sana na kilichotokea baada ya hapo, furaha ambayo niliiona kwa mashabiki ilinishangaza sana.

“Unajua suala la ushindi linamgusa shabiki yeyote ambaye anakuwa amekwenda uwanjani. Lakini hawa wa Yanga walinishangaza, walikuwa wamefurahi sana, walionyesha kuwa furaha yao imezidi kipimo na kweli, nilibaki sina cha kusema.


“Mfano, baada ya mechi kuisha, wachezaji tulikuwa na furaha sana, baadaye niliona viongozi wa Yanga wakija vyumbani, Injinia Hersi alikuja chumba cha kubadilishia nguo akiimba na kucheza. Kabla sikuwa nimewahi kumuona akifanya hivyo lakini alikuwa na furaha na faraja ya kupita kiasi.


“Kule Afrika Kusini mara kadhaa tulishinda dhidi ya Kaizer Chiefs lakini haikuwa vile. Mara nyingi furaha yao itaonekana mitandaoni lakini kwa hapa Tanzania, kazi inaanzia pale uwanjani.

 Mashabiki wa Tanzania kwa kweli wanapenda mpira lakini mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiendelea kunishangaza.”

Morisson bado anataka mafanikio akiwa na Yanga ambayo ameongeza nayo mkataba wa miaka miwili ingawa naye ameendelea kukiri kwamba hawana nafasi ya kubeba ubingwa wa Bara kwa msimu huu kwa kuwa hawaamini wanaweza vipi Simba kufanya makosa ya mfululizo hadi kuukosa ubingwa.


Kwa sasa Ligi Kuu Bara imesimama kutokana na vita dhidi ya ugonjwa wa Corona.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.