WAKATI Yanga wakiwa wanafanya usajili wao wa dirisha dogo, mabosi wa Simba wenyewe walikuwa wanazunguka huku na kule kwa ajili ya kumalizana na watu, sasa wameibuka na kuweka bayana balaa lao la kutambulisha vifaa vyao linaanza leo Jumatatu.
Simba wanaanza kutambulisha vifaa vyao baada ya Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Senzo Mazingisa raia wa Afrika Kusini kuweka bayana kwamba wanamalizana vitu vidogo na wachezaji waliowasajili kisha wanaanza kuwatambulisha.
Miongoni mwa wachezaji ambao wanaweza kutambulishwa katika usajili mpya wa Simba ni kiungo mshambuliaji LuÃs Jose Miquissone ambaye anaichezea UD do Songo kwa mkopo huku akiwa mali ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Nyota huyu alikuwa karibu kabisa kutua Jangwani lakini Simba wameipindua Yanga kwa kumfuata na donge nono zaidi ambalo Senzo hakutaka kuliweka wazi.
Senzo hivi karibuni alikuwa Afrika Kusini kwa ajili kukamilisha usajili wa nyota kadhaa akiwemo Luis ambaye Yanga imenyanganywa tonge mdomoni.
Nyota huyo alikuwa ameshazungumza na kukubaliana kila kitu na Yanga lakini Simba walipomfuata akabadili gia hewani. Na sasa Championi Jumatatu linajua kuwa anakaribia kusaini mkataba wa miaka miwili Msimbazi.
Senzo ameliambia Championi Jumatatu, kuwa wataanza kushusha vifaa vyao vipya wiki hii kuanzia leo Jumatatu ikiwa ni baada ya kumalizana navyo huku wengine wakiwa kwenye hatua ya mwisho ya kuwasainisha.
Msauzi huyo aliongezea kuwa walichelewa kuanza kufanya usajili katika kipindi hiki kutokana na kutaka kumpa muda kocha wao mpya Sven Vanderbroeck awatajie ni sehemu gani ambayo anaona anahitaji kuongeza mtu.
“Wiki hii inayoanza kesho (leo) Jumatatu tutatambulisha wachezaji wetu ambao tumewasajili katika dirisha hili dogo baada ya kumalizana nao kwa kila kitu. Walikuwa wengi ndiyo maana imekuwa ngumu kutangaza mapema ni kina nani ambao tumewasajili.
“Lakini kitu kingine tulikuwa tunasubiri kujadiliana na mwalimu ni nani na nani wasajiliwe na katika nafasi zipi ndiyo maana tulikuwa kimya kidogo, lakini wiki hiyo inayoanza keshokutwa (jana) Jumatatu basi ndiyo tutatangaza watu wote ambao tumewasajili.
“Kuhusiana na suala hilo la huyo Luis hatuwezi kuliweka wazi sana kitu cha msingi ni kusubiri kuona kwamba nani tutamtangaza, lakini pia kuna wachezaji wengine watatu nao wamekuwa wakihusishwa sana na sisi ila hatuwezi kuwazungumzia hadi pale ambapo tutamalizana nao kabisa,” alisema Senzo
Post a Comment