PASCAL Wawa, beki kisiki wa Simba, amesema anataka kuona Simba inasajili watu wa kazi kwa ajili ya msimu ujao katika kila nafasi ikiwemo nafasi yake ya ulinzi.
Imekuwa ikielezwa kuwa, Simba ipo kwenye mchakato wa kuwavuta mabeki wawili wa maana kutoka Coastal Union ambao ni Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Ame kwa ajili ya msimu ujao.
Wawa alisema kuwa anafurahia kuona akiwa na wachezaji wapya ndani ya kikosi cha Simba kwani wengi waliosajiliwa wanafanya vizuri kwa manufaa ya timu.
“Hata wakiletwa mabeki wawili ama watatu waje tu Simba, huwezi kuzuia klabu kufanya usajili na kwa namna ambavyo unapata changamoto unakuwa bora zaidi, hilo ni jambo zuri iwapo litatimia.
“Ninapenda kuona kwamba wakati wa usajili klabu inasajili wachezaji wazuri ambao watakuwa na nafasi ya kutimiza majukumu yao kama ambavyo wanafanya wengine ambao wamesajiliwa hapa,” amesema Wawa raia wa Ivory Coast.
Katika kikosi cha Simba, msimu huu kabla ya kuanza kwa ligi, walisajiliwa mabeki wa kati wawili ambao Tairone Santos raia wa Brazil na Kennedy Juma.
Ukiwaondoa mabeki hao wawili wa kati, wengine wanaocheza nafasi hiyo ndani ya Simba ni Erasto Nyoni, Yusuf Mlipili na Wawa.
Wakati Wawa akisema hivyo, kocha wake mkuu, Sven Vandenbroeck raia wa Ubelgiji, alisema anataka kusajili wachezaji ambao wakiingia kikosini watakuwa tayari kucheza moja kwa moja na si kupewa muda wa kuzoea mazingira.
Chanzo: SpotiXtra
Post a Comment