UONGOZI wa Yanga umefichua kuwa mbinu pekee itakayowarudisha kushiriki michuano ya kimataifa ni kutwaa taji la Kombe la Shirikisho ambalo lipo mikononi mwa Azam FC kwa kushinda mechi zote itakazocheza.
Kwenye Kombe la Shirikisho, Yanga ipo hatua ya robo fainali na bingwa wa kombe hilo huiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa mkakati mkubwa ni kuona timu inafikia malengo yao ikiwa ni pamoja na kushiriki michuano ya kimataifa.
“Tunahitaji kubeba taji la Kombe la Shirikisho na njia ni moja tu kushinda mechi zote tutakazocheza kuanzia pale tutakapokuwa ndani ya uwanja, iwapo tutashinda mechi zote tutakazocheza matokeo yake itakuwa ni kutwaa kombe na kurejea kwenye michuano ya kimataifa hakuna jambo lingine tunalofikiria,” amesema Bumbuli.
Timu nane zilitinga hatua ya robo fainali ambazo ni Yanga yenyewe pamoja na Alliance FC, Azam FC, Kagera Sugar, Namungo FC, Ndanda FC na Simba zinazoshiriki Ligi Kuu Bara na Sahare All Stars inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ratiba inatarajiwa kupangwa leo.
Post a Comment