KILIO cha wengi awali ilikuwa ni kuona kwamba mambo yanatulia na masuala ya michezo yanaendelea ili wanafamilia ya michezo wapate burudani ambayo walikuwa wameikosa.
Ilikuwa ni ngumu kujua kwamba mambo yatakuwa shwari lini kwani presha ilikuwa kubwa na kila mmoja alikuwa na mashaka kuhusu hatma ya masuala ya michezo hasa ukizingatia kwamba kuna wengine waliamua kufuta kabisa matokeo ya mechi zote.
Yote haya yalisababishwa na janga la Virusi vya Corona ambavyo vinaivurugavuruga dunia namna vinavyotaka lakini sasa kumeanza kuwa na nafuu kidogo licha ya vurugu zake kuendelea kuishi.
Nikukumbushe kuwa Machi 17 Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ilitangaza kusimamisha shughuli zote zisizo za lazima ikiwa ni pamoja na masuala ya michezo.
Huku iligusiwa michezo yote kuanzia Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na la Pili, Ligi ya Wanawake pamoja na ligi za mikoa bila kusahau ile ya mchangani ilisimamishwa.
Lengo kubwa ilikuwa ni kupunguza maambukizi zaidi ya Virusi vya Corona ambavyo wataalamu wanaeleza kuwa vinasambazwa kwa njia ya hewa hivyo ilikuwa ni lazima kuchukua tahadhari.
Baada ya vita ya muda kupita sasa Serikali imeona kwamba kuna unafuu ambao unaweza kufanya shughuli zikaendelea ikiwa ni pamoja na masuala ya michezo.
Tayari mwanga umeanza kuonekana baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kusema kuwa anaruhusu shughuli za michezo kurejea kuanzia Juni Mosi.
Jambo jema na linapokelewa kwa mikono miwili na familia ya michezo kwani hakuna ambaye alikuwa hajaukumbuka mpira hata mimi nilikuwa nimeukumbuka pia.
Sasa tatizo lingine limeibuka ambapo kila mmoja kwa sasa anavutia kamba kwake akihitaji kupata wepesi kulingana na namna ligi inavyokwenda kumalizika.
Tayari Serikali imesema kuwa ligi itamalizka kwa kuchezwa kwenye vituo viwili ambapo kimoja kipo Dar es Salaam na kingine kipo Mwanza.
Mgawanyo wa vituo hivi upo namna hii kile cha Dar kitakuwa kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu Bara pamoja na zile za Kombe la Shirikisho huku kile cha Mwanza huko ni mwendo wa Ligi Daraja la Kwanza na la Pili.
Wapo wanafamilia ya michezo wamevitazama vituo na kuanza kuumia moyoni kwa kuwa hawatakuwa na zile mechi zao za nyumbani kwa sasa hasa ukizingatia watakuwa sehemu moja.
Hapa ndipo maajabu yapo wale ambao walikuwa wanauliza ligi itarejea lini ili apatikane mshindi halali wanafikiria kuhusu mechi zao za nyumbani na huko ndiko wanapeleka malalamiko yao wakidhani wanaonewa.
Ukiachana na hao pia wapo wale wanaopenda kuona ligi ya Wanawake ikirejea kwani ni ligi tatu zimeruhusiwa nao wanaamini kuwa wametengwa kisa hawataanza kucheza kwa sasa.
Hapana kwa sasa vilio hivi inatosha ni lazima kila mmoja ajipange kwa ajili ya ligi na ratiba itakapotoka msimu uiishe kwa amani na bingwa apatikane.
Tunajua kwamba zipo timu ambazo zilikuwa zinategemea mechi za nyumbani ili kupata ushindi na kipato hilo inabidi lipite tu kwa sasa.
Ile imani kwamba Simba, Azam FC, KMC na Yanga mechi zao nyingi zitakuwa ni za nyumbani kwa sasa hakuna namna ya kuzuia kwani janga la Corona ndilo limesababisha haya tuache yapite.
Wengine wanaamini kwamba hali hiyo inawapelekea ubingwa mapema Simba kwa kuwa mechi nyingi watacheza wakiwa nyumbai hilo sio kweli, mshindi ni baada ya dakika tisini.
Hakuna aliyetengwa kwa upande wa Wanawake na ligi nyingine ambazo hazijaruhusiwa kuanza wala anayependelewa imani yangu ni kwamba mambo yakiwa sawa ligi zote zitarejeshwa ila kwa sasa tahadhari ni muhimu kuchukuliwa
Post a Comment