KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, raia wa Ubelgiji amefunguka kwamba licha ya Serikali kuruhusu michezo lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanatakiwa kutoa muda kwa ajili ya timu kupata nafasi ya kufanya mazoezi ya pamoja.
Kocha huyo amedokeza kwamba hawawezi kurejea na kuanza kucheza ligi Juni Mosi ambapo michezo imeruhusiwa kwa sababu hawakuwa kwa muda mrefu, hivyo wanahitaji tena muda mfupi wa maandalizi kabla ya ligi kuanza.
Serikali imeruhusu kuendelea kwa shughuli za kimichezo nchini. Michezo yote ya ligi kuu iliyobakia itapigwa kwenye viwanja vya Dar; Uhuru, Taifa na Azam Complex.
Eymael amesema kuwa ni muhimu kwa TFF kutoa muda huo kama wanataka ligi iishe kwa ushindani, kwa sababu itarudisha muunganiko wa wachezaji ambao hawajakaa pamoja kwa muda wa miezi miwili.
“Kitu kizuri ni kwamba ligi inarudi tena lakini napendekeza kwamba kabla ya kuanza tena kutolewe kwa muda kwa ajili ya timu kufanya mazoezi kwa pamoja.
“Nimeambiwa ratiba inaweza kuanza Juni 15, ikiwa hivyo ni kitu kizuri kwa sababu kutakuwa na muda wa timu kukaa pamoja na kufanya mazoezi na jambo hilo litafanya kuwe na ushindani kama ilivyokuwa awali,” alimaliza Eymael
Post a Comment