Na Saleh Ally
HAJI Manara ni mtaalamu sana katika suala la propaganda, anajua afanye nini kwa wakati gani, acheze na kipi kuhusiana na jambo husika katika wakati husika ili aweze kufanikiwa.
Kwa kifupi, Manara ni mwanasiasa ingawa ni mtu anayeupenda mpira na kweli kama anavyosema yeye amekuwa kati yaw ala wachambuzi wa mwanzo kabisa katika masuala ya soka.
Kwa kuwa alisomeshwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) katika masuala hayo ya propaganda, amepata nafasi kubwa sana ya kujifunza mengi katika siasa na mara nyingi nikizungumza naye, namuona ndoto yake kuu ni kuwa mwanasiasa mkubwa au kufanikiwa kupitia nyanja hiyo.
Huenda akawa anasita kutokana na mafanikio yake Simba lakini ninaamini siku moja lazima ataingia katika jambo la siasa hata kama ataamua kubaki Simba.
Nimepata bahati ya kufanya kazi na Manara wakati huo nikiwa mwandishi chipukizi kabisa. Nakumbuka ilikuwa mwanzoni mwa miaka yangu mitano ya uandishi wa habari, wakati huo akiwa Radio One na baadaye Radio Uhuru, bila ya ubishi hata kama anakosea vipi, pamoja na elimu ya propaganda lakini Manara ana uwezo mkubwa sana katika uzungumzaji.
Unapokuwa naye karibu lazima uwe makini kwa kila analozungumza au unalotaka kuzungumza. Kipaji cha kuyachezea na kuyageuza maneno au kuzipandia na kuzishusha hoja ni mkubwa. Hiki ni kipawa ambacho ni baraka kutoka kwa MWenyezi Mungu.
Binafsi navutiwa kuendeleza vile ambavyo naona tayari Mungu ameamua view bora au vikubwa kwa kuwa ni sehemu ya utukufu wake. Nimekuwa nikiwaza alipofikia Manara na kumuombea asibweteke, asijisahau na kusahau alipotoka lakini bila ya ubishi ana kitu kikubwa kakifanya katika mpira tunapaswa kumkubali na kumpongeza.
Sisemi Manara asikosolewe, au kila atakachosema ni sawa. Mimi mwenyewe kama ataleta mchezo, sitakaa kimya lakini nataka tuhamie katika utamaduni wa kukubali ubora na mazuri ya wenzetu katika jamii.
Nasema hivyo kwa kuwa nimemsikia Manara wakati akifanya mahojiano katika runinga moja akisema kwamba kuna viongozi ndani ya Simba wamekuwa wakifanya mambo yakiwemo ya kutaka kumuangusha.
Anaamini kiongozi au viongozi hao walichangia yeye kuwekwa ndani baada ya Mkurugenzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji kutekwa na watu wasiojulikana.
Manara anaamini kumekuwa na fitina na figisu nyingi baina yake na kiongozi huyo kwa kuwa tu, suala ni umaarufu. Maana yake ndani ya Simba kuna viongozi wanakerwa na umaarufu wake.
Katika maisha ya kawaida ya Kitanzania hili jambo lipo karibu kila sehemu na hakika si zuri. Kwa kiasi kikubwa limekwamisha mambo mengi sana ya maisha yetu, wengi wakionekana kukerwa na umaarufu wa watu wao wa karibu wakitaka kuuzuia au kuhakikisha hauendelei ambalo ni jambo la upotezaji wa muda kwa kiasi kikubwa.
Kama kuna viongozi wanamfanyia hivyo Manara, hakika hata mimi natamani kuwafahamu. Mwenyewe amesema kuna siku atawataja, natamani hiyo siku ifike ili tujifunze jambo na kama ni hivyo ni kosa kubwa sana.
Manara ataendelea kubaki na nafasi yake hadi atakapoondika Simba, iko siku naye atapita kama walivyopita watu wengine, jambo ambalo ni la kawaida kabisa.
Kiongozi anayemuonea wivu Manara, naye ana nafasi yake lakini akumbuke pia hatadumu milele. Kuna siku lazima naye ataondoka Simba, iwe kwa kupenda au tofauti kwa kuwa ni mwanadamu.
Hivyo ni vizuri sana kila mmoja kumpa nafasi mwingine ili aweze kutumia kipawa au uwezo alionao kukijenga kile ambacho mnakuwa mnakiongoza badala ya kuwa unaumizwa na mafanikio ya mwenzako.
Inawezekana wewe una uwezo wa kupendeza kama kiongozi kwa kuvaa suti nzuri, kutengeneza nywele kwa ufasaha na ikiwezekana muonekano wa bashasha, likawa jambo linalowavutia watu. Lakini Manara yote hayo hana, mdomo wake ndio silaha, uwezo wa kuzungumza ndio ujenzi wa upendo kwa watu wa Simba.
Kama ainaifanya kazi yake vizuri, basi munge mkono, nawe endelea kuwa na aina yako, pendeza, zungumza vizuri kwa mapozi lakini huenda una jambo jingine katika sehemu ya kuendeleza klabu yenu, Manara naye asikuzuie, basi Simba itaendelea kupiga hatua kupitia kipawa au uwezo wa kila mmoja.
Haya mambo ya roho mbaya yamepitwa sana na wakati na kama kweli yapo, kwa viongozi ingawa hatujamjua ni nani, basi vizuri kuachana nayo na mwenye tabia kama hiyo naye aache kwa kuwa Simba haiwezi kujengwa na mtu mmoja au aina ya mtu mmoja au watu wanaofanana tu badala yake aina tofauti ya watu kwa maana ya elimu, busara, vipaji na kadhalika ambavyo vinatengeneza umoja wenye nguvu katika maisha ya klabu husika.
Ungeniambia nimpe Manara ushauri, ningemuambia aanchane huyo kiongozi asimtaje kwa maslahi ya Simba kwa kuwa kamwe hana uwezo wa kumzuia, zaidi ya kumpotezea muda. Ingawa kama ataona anazidi, hataki kusikia na anaamini umaarufu ndio maisha, basi atamje tu ili tumtumie kama darasa kuwafundisha wengine
Post a Comment