LUC Eymael, Kocha Mkuu wa Yanga ameweka wazi kwamba katika kikosi chake cha msimu ujao atakachofanya ni kutosajili wachezaji wengi badala yake atafanya maboresho kidogo.
Eymael raia wa Ubelgiji, amefunguka kwamba hahitaji wachezaji wengi katika kikosi chake cha msimu ujao badala yake analenga kuchukua wachezaji wachache ambao watakuja kuongeza nguvu kwa waliopo sasa.
Eymael ameongeza kwamba hatafanya kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo kikosi hicho kilisajili zaidi ya wachezaji 11 kwenye dirisha kubwa la usajili wakati kocha mkuu akiwa Mwinyi Zahera raia wa DR Congo.
Kocha huyo amesema, kuwa mipango yake kwa sasa ni kuongeza nguvu mpya za wachezaji wachache katika wale ambao wamebakia kwa ajili ya kuifanya timu hiyo kwa msimu ujao kuwa na nguvu ya kupambana.
“Ripoti juu ya nani na nani wasajiliwe tayari niliiwasilisha kwa viongozi na kuweka wazi kwamba nahitaji nafasi hizi na hizi katika kikosi cha msimu ujao.
“Nitakachofanya ni kutokuwa na kundi kubwa la wachezaji kwa sababu kuna wengi ambao wapo kikosini kwa sasa nimewaona wanaweza kutusaidia, kwa hiyo ni kuwaongezea kiasi kidogo cha wachezaji kisha wafanye kazi.
“Nataka kujenga kikosi imara kwa hiyo sitaweza kusajili namba kubwa ya wachezaji badala yake nitawaboreshea kwenye maeneo kadhaa kisha tutakuwa tayari kupambana,” alimaliza Mbelgiji huyo.
Miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa na Yanga katika usajili wa dirisha kubwa msimu huu na kuachwa ni Juma Balinya, Sadney Urikhob, Maybin Kalengo na Mustafa Seleman ambao walionekana kushindwa kufi kia malengo.
Post a Comment