MICHAEL Sarpong, mshambuliaji wa zamani wa Rayon Sports ya Rwanda, ambaye hivi sasa ni huru anatua kuichezea Yanga katika kuelekea msimu ujao.
Mshambuliaji huyo raia wa Ghana, hivi karibuni mkataba wake ulivunjwa na Rayon kwa kile kilichoelezwa kuongoza mgomo wa wachezaji wakidai malipo ya mshahara wa mwezi Machi, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael, mshambuliaji huyo ana sifa zote ambazo anazozitaka yeye, hivyo ana nafasi kubwa ya kutua kujiunga na Yanga katika msimu ujao.
Eymael aliitaja moja ya sifa hizo ni ujasiri aliokuwa nao wa kupambana bila ya kuwaogopa mabeki watukutu na watemi wa timu pinzani, jambo ambalo linamfanya aamini kuwa ni mtu sahihi kwenye timu hiyo.
“Sarpong yupo kwenye mipango yangu ya usajili katika msimu ujao, ninaamini viongozi hawatashindwana naye kwani ni mchezaji huru hivi sasa na uzuri tayari nimeanza mazungumzo na meneja wake.
“Na kama mazungumzo yakienda vizuri, basi atakuja Yanga kwani ni kati ya washambuliaji wenye sifa zote ambazo mimi ninazihitaji awe nazo mshambuliaji.
“Nimekuwa nikimfuatilia kwa karibu, hivyo ninamjua vizuri sina hofu ya uwezo wake, ninafanya mawasiliano na meneja wake kila kitu kinakwenda vizuri,” amesema Eymael
Post a Comment