BEKI wa pembeni wa zamani wa Yanga, Hassan Kessy, amesema kuwa kama klabu yake hiyo ya zamani ikifanikiwa kunasa saini ya beki wa kati wa Nkana Rangers ya Zambia, Mussa Mohammed, itakuwa imepata jembe.
Mussa ni kati ya mabeki wa kati wanaotarajiwa kujiunga na Yanga katika msimu ujao huku taarifa zikienea kuwa mabosi wa timu hiyo wapo kwenye mazungumzo ya awali na beki huyo.
Yanga imepanga kuifanyia maboresho safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji kwa mujibu wa ripoti ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Luc Eymael.
Kessy amesema anafahamu uwezo wa beki huyo anayecheza naye Nkana, hivyo anaamini kama Yanga ikifanikiwa kumsajili, basi watakuwa wamesajili beki mzuri kutokana na kiwango chake kikubwa alichonacho.
Kessy amesema kuwa kati ya mabeki bora wa kati Zambia, Mussa ni miongoni mwao kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupambana na washambuliaji hatari wa kufumania nyavu. Aliongeza kuwa beki huyo ni chaguo bora kama kweli Yanga wanahitaji beki wa kati huku akiwashauri kumalizana na staa huyo wa Nkana haraka kama kweli wanamhitaji.
“Nimesikia tetesi za Yanga kumhitaji beki mwenzangu wa Nkana, Mussa kama kweli wanamuhitaji, binafsi nampitisha katika usajili wao na hiyo ni kutokana na kufahamu uwezo wake.
“Kwa wachezaji Watanzania wanaocheza hapa Zambia, wanafahamu uwezo wake, kwani ni kati ya mabeki bora katika Ligi Kuu ya Zambia, binafsi sina hofu na uwezo wake.
“Mussa ni beki mbishi, mpambanaji ambaye ni mbishi kukubali kupitwa kirahisi, hivyo kama akijiunga na Yanga basi utakuwa usajili bora katika safu ya ulinzi wa kati,” alisema Kessy ambaye ni mchezaji huru.
Chanzo: Championi
Post a Comment