AMIS Tambwe, mshambuliaji wa zamani wa Yanga, amesema kuwa anaamini ni majungu tu ya watu wasiopenda mafanikio yake, ndiyo yalichangia yeye kuondoka ndani ya Yanga na siyo kuchuja kwa uwezo wake.
Tambwe alikipiga Yanga msimu wa 2018/19 chini ya Kocha Mkuu Mwinyi Zahera na aliibukia Klabu ya Fanja FC ya Oman ambayo amevunja nayo mkataba na kwa sasa yupo zake Burundi.
Tambwe amesema kuwa bado alikuwa kwenye ubora wake kwani licha ya kupewa muda mchache uwanjani, alikuwa akiwaonyesha kwa vitendo kwamba anaweza kazi.
“Nadhani labda ni majungu tu yaliniondoa Yanga ila ukisema ni uwezo wangu kuchuja ama kupungua hilo siamini, ninakwambia hivyo kwa sababu nilipata muda mchache wa kucheza ila nilifunga mabao mengi.
“Mabao 12 ujue sio ya kubeza kufunga, hapo sikuwa namaliza dakika zote tisini, unadhani nini kingetokea kama ningemaliza dakika zote tisini? Bado nipo imara na ninaweza kucheza popote na kutimiza majukumu yangu,” amesema.
Tambwe alifunga mabao nane ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19 na mabao manne alifunga kwenye Kombe la shirikisho.
Kabla ya hapo, aliichezea Yanga msimu wa 2015-16 na kuibuka mfungaji bora akifunga mabao 21. Aliwahi pia kuwa mfungaji bora simba msimu wa 2013/14 akifunga mabao 19
Post a Comment