UONGOZI wa Yanga umepanga kuwarejesha makocha wake, Mbelgiji, Luc Eymael na msaidizi wake raia wa Afrika Kusini, Riedoh Berdien waliopo nje ya nchi baada ya Serikali kutangaza kurejesha michezo ikiwemo Ligi Kuu Bara kuania Juni Mosi, mwaka huu.
Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli, ametangaza uamuzi huo juzi jijini Dodoma wakati akiwaapisha viongozi wateule mbalimbali katika hafl a iliyofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani humo.
Ligi ilisimama tangu Machi 17, mwaka huu ili kupisha Virusi vya Corona baada ya Waziri Mkuu ya Tanzania, Kassim Majaliwa kutoa tamko la kusimama kwa michezo yote ikiwemo soka.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, amesema,wamepanga kuwatumia tiketi za ndege makocha hao haraka baada ya Rais kutangaza kuruhusu ndege kutoka mataifa mengine kuanza kuingia nchini.
Aliongeza kuwa hivi sasa wanaangalia ndege gani itakayomfaa kocha huyo kumfikisha nchini ili kuungana na kikosi cha timu hiyo kitakachokuwa chini ya Charles Mkwasa.
“Tumepokea kwa mikono miwili taarifa za kurejea kwa michezo, hivyo tunaamini ligi itaendelea ili kumalizia michezo tuliyoibakisha kabla ya kuuanza msimu mpya.
“Hivyo, tumepanga kuwakatia tiketi makocha wetu haraka baada ya Rais kutangaza kuwa ndege kutoka mataifa mengine zitaanza kuruhusiwa kuingia nchini.
“Tutaangalia ndege gani itamfaa na kocha wetu ambaye tumepanga atarejea nchini ndani ya hizi siku tatu kuanzia kesho (jana) kwa ajili ya kuungana na kikosi chake kuendelea na maandalizi,” amesema Mwakalebela.
Eymael naye alipotafutwa kuzungumzia hilo alisema: “Nimeshukuru kusikia ndege zimeanza kuruhusiwa kuingia Tanzania, binafsi nimefarijika mipango ya safari ikikamilika nitarudi kuendelea na ligi, lengo ni kuipa mafanikio klabu yangu ya Yanga kwa kushika nafasi za juu katika msimamo wa ligi, tuombe taratibu zikamilike kila kitu kitakuwa sawa.”
Post a Comment