HASSAN Dilunga, kiungo mshambuliaji wa Simba amewaaga mabosi wa klabu hiyo baada ya kutamka kwamba kwa msimu ujao ndoto zake ni kwenda kutafuta changamoto mpya.
Kiungo huyo ametamka kwamba akili yake ni kuwa muda wake ukimalizika kikosini hapo ni kwenda nje kwa ajili ya kusaka maisha mapya ambapo meneja wake anashughulikia suala hilo kwa sasa.
Dilunga ni miongoni mwa wachezaji ambao wanamaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu ambapo amekuwa na kiwango kizuri kikosini hapo chini ya Mbelgiji Sven Vandenbroeck.
Kiungo huyo amesema kwamba licha ya kwamba ana mkataba na Simba hadi sasa ni kuwa malengo yake ni kuvuka kutoka mahali ambapo alipo na kwenda sehemu nyingine ambapo suala zima lipo mikononi mwa meneja wake.
“Kila mtu anafanya kazi avuke pale alipo, anahitaji atoke hapa aende pale na kitu kikubwa ni kumuachia Mungu kila kitu kiende salama.
“Kila mchezaji ana malengo ya kwenda mbali, naimani huu ndiyo wakati wangu, nishaongea na meneja ili tutoke kidogo, nataka kutoka Tanzania na kwenda kwingine japo siwezi kusema niende huku wala kule ila ikitokea nchi yoyote nitapata nafasi ya kwenda basi sawa.
“Mimi bado niko Simba ila lolote linaweza kutokea kwangu na maisha ya hapa Simba lakini kwa sasa hivi ligi inatakiwa kuendelea,” alimaliza HD.
Post a Comment