MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu za Simba na Yanga, Mrundi Amiss Tambwe amefunguka kuwa bado ana ndoto za kurejea Yanga.
Tambwe anasema katika moyo wake ameiweka klabu ya Yanga kwa sababu ilimfanyia makubwa katika historia yake ya soka, hivyo itakuwa busara na furaha kwake kama ikitokea akapata nafasi ya kurudi tena na kuitumikia.
Tambwe alidumu Yanga kwa misimu minne na kufunga zaidi ya mabao 50 na kuwa moja ya wachezaji waliovuna mafanikio, lakini msimu uliopita alitupiwa virago na kujiunga na Fanja FC ya Oman, ambayo nayo alivunja nayo mkataba na kurudi kwao Burundi akiwa mchezaji huru hadi sasa.
Tambwe amesema wapo watu ambao wanataka astaafu kucheza soka kwa kuwa umri wake umekwenda, jambo ambalo anasema siyo sahihi kwa kuwa bado ana nguvu ya kucheza soka la ushindani kwa miaka minne zaidi.
“Kusema ukweli bado nina mapenzi na Klabu ya Yanga, ile timu ilibadilisha maisha yangu na kunipa historia kubwa, hivyo natamani nirudi tena na nicheze pale hadi nitakapostaafu.
"Watu wanasema niache soka umri wangu umekwenda, jambo ambalo siyo kweli, mimi nina miaka minne zaidi ya kucheza na ndiyo maana nasema natamani kurudi Yanga,” amesema Tambwe.
Post a Comment