HABARI njema kwa wapenda soka Ujerumani na duniani kote ni kwamba, Ligi Kuu ya Uejrumani maarufu Bundesliga inarejea na mechi zake zinatarajiwa kuchezwa katikati ya mwezi huu.
Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali ya Ujerumani kutangaza sasa ligi zinaweza kurudi kuchezwa nchini humo.
Bundesliga ilisimama katikati ya Machi, mwaka huu baada ya kusambaa kwa kasi virusi vya corona ambavyo kwa Ujerumani vimeathiri zaidi ya watu 150,000, huku takribani watu 6,300 wakifariki nchini humo.
Tangu kuwepo kwa corona, Bundesliga inakuwa ligi ya kwanza Ulaya kurudi kuchezwa, huku Uholanzi na Ufaransa wenyewe wakimaliza ligi zao za msimu huu.
Kesho Alhamisi, kikao cha Bundesliga kitafanyika kwenye Mji wa Frankfurt kuangalia hali ya afya itakuwaje, huku pia kukipangwa tarehe rasmi ya kuendelea kwa msimu huo.
Wakati Bundesliga inasimama, klabu nyingi zilikuwa zimebakiwa na mechi takribani tisa kumaliza msimu huu, huku Eintracht Frankfurt na Werder Bremen zikibakiwa na mechi kumi kila moja.
Vinara Bayern Munich wamewaacha Borussia Dortmund kwa pointi nne.
Lakini ligi hiyo itarudi ikiwa chini ya uangalizi maalum kutokana na hivi karibuni Klabu ya FC Cologne kuripoti kuwa na wagonjwa watatu wa corona
Post a Comment